Habari MsetoSiasa

Mudavadi na Weta watakiwa kujiunga na Jubilee

June 5th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wa Jubilee kutoka magharibi mwa Kenya wamewataka vinara wa NASA Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula ‘kuondoka kwenye baridi’ na kujiunga na serikali.

Mbw Emmanuel Wangwe (Navakholo), Dan Wanyama (Webuye Magharibi) na Didmus Barasa (Kimilili) waliwataka wawili hao kuiga mfano wa wenzao Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kwa kufanya kazi na Rais Uhuru Kenyatta.

“Kalonzo alihudhuria Maombi ya Kitaifa na kuwasalimiana na Naibu Rais William Ruto na Bw Odinga licha ya kuachwa nje katika mwafaka wa hapo awali. Sasa Musalia na Wetang’ula hawana budi kujiunga kufuata nyayo za wenzao na kujiunga na Jubilee,” akasema Bw Wangwe.

Naye Bw Wanyama alisema endapo wawili hao wanajiunga na serikali watajiweka katika nafasi nzuri kupata vyeo vya juu katika uchaguzi wa mwaka wa 2022.

“Ikiwa Mudavadi na Wetang’ula watajiunga na serikali watakuwa katika nafasi bora kujadiliana na Naibu Rais William na viongozi kutoka maeneo mengine katika siasa zijazo,” akasema.

Kwa upande wake Bw Barasa alisema njia ya kipekee ya Mudavadi na Wetang’ula kumpinga Raila chenga kisiasa ni kushirikiana na Rais Kenyatta na naibu wake Ruto katika mipango yao ya kuwahudumia Wakenya.

“Njama fiche za Raila zitaambulia patupu ikiwa viongozi hawa wawili watajiunga na serikali katika mchakato wake wa kuunganisha nchi kwa ajili ya maendeleo. Kupitia njia hiyo sisi kama Waluhya tutafaidi,” akasema Bw Barasa ambaye anahudumu muhula wake wa kwanza.

Wabunge hao watatu walikuwa wakiongea Jumamosi katika hafla ya mazishi katika eneo bunge la Navakholo.

Mbw Mudavadi na Wetang’ula hawakuhudhuria hafla ya maombi ya kitaifa katika mkahawa wa Safari Park, Nairobi. Hata hivyo, Bw Musyoka aliwataka Rais Kenyatta na Bw Odinga kuhusisha wawili hao katika mchakato wa kuunganisha taifa.

“Leo ni siku muhimu zaidi kwa sababu sisi kama viongozi tumeungana hapa kwa ajili ya kupalilia umoja na uthabiti wa taifa letu. Ingekuwa bora zaidi ikiwa wenzetu, Mudavadi na Weta pia watajumuishwa katika mchakato huu ili sote tutembee pamoja,” akasema kiongozi huyo wa chama cha Wiper.