Habari MsetoSiasa

Mudavadi sasa ataka kubuni NASA mpya

September 30th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU

KIONGOZI wa chama cha Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi amefichua mpango wa kuunda muungano mpya wa NASA anapojitayarisha kuwania urais mnamo 2022.

Bw Mudavadi (pichani) alisema NASA haikuwa chombo bali wazo la kukomboa Kenya, na hivyo basi azimio la NASA haliwezi kuangamia kwa hivyo ataanza kuzunguka kote nchini na kimataifa kushawishi Wakenya kuungana naye anapojitahidi kuanzisha muungano wa ‘Kenyan National Super Alliance.’

Akihutubu Jumamosi kwa Wakenya wanaoishi katika jimbo la New Jersey, Amerika, Bw Mudavadi alisema muungano aina hiyo ungali ndio njia pekee ambapo Kenya itajikomboa kutoka changamoto zinazoikumba.

“Najua kwamba watu wengi hawakuelewa maana halisi ya muungano wa NASA. Muungano ninaodhamiria kuuhusu si wa wanasiasa kushirikiana kutafuta nyadhifa za uongozi. Ni muungano wa Wakenya wanaoipenda nchi yao. Ni muungano wa Wakenya wanaoamini kuwa Kenya inaweza kukombolewa na kuwa nchi ya matumaini,” akasema Bw Mudavadi.

Kumekuwa na dhana kuwa muungano huo ulisambaratika, hasa baada ya kiongozi wa ODM Raila Odinga kubuni handisheki na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018 bila kuwaarifu vinara wenzake.

Muungano huo ulivishirikisha vyama vya ODM, ANC, Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka na Ford-Kenya chake Seneta Moses Wetang’ula (Bungoma).

Viongozi hao walianza kulaumiana wao kwa wao, wakidai kuwa kinara wa ODM Bw Odinga alifanya kinyume na mUafaka waliokubaliana.

Migawanyiko katika muungano huo imedhihirika wazi katika kinyang’anyiro cha ubunge kwenye uchaguzi mdogo wa Kibra, ambapo vyama hivyo vimesimamisha wawaniaji mbalimbali.

ODM imemsimamisha Bw Imran Okoth, ANC imemsimamisha Bw Eliud Owalo ambaye alihama ODM huku Ford-Kenya ikimsimamisha Khamisi Butichi.

Chama cha Wiper kilikuwa kimetangaza kumsimamisha mwanamuziki Jackson Ngechu maarufu kama “Prezzo” lakini kikafutilia mbali mpango huo.

Tayari, ODM imelalama “kusalitiwa” na vyama hivyo, ikidai kuwa vinalenga kumnyima mwaniaji wake ushindi.

Lakini Bw Mudavadi amepuuzilia mbali wanaotishia kuvunja NASA akisema wale wanaotaka kuondoka wako huru kufanya hivyo.

“Waliokufa moyo wanaweza kuondoka lakini nitasimama imara kwa maono ya NASA. Ninatoa wito kwa Wakenya walio ughaibuni na walio nyumbani waungane nami,” akasema.

Alieleza kuwa muungano huo hautayumba, hata ikiwa wanachama wake watauhama na kubaki wanachama wawili pekee.

“Nitazuru kila mahali kuuza ndoto yangu jipya kupitia NASA. Kutoka leo, sitaki kuulizwa ikiwa NASA ipo ama haipo. NASA ni maono ya kuikomboa Kenya. Ndoto hiyo haiwezi kufa,” akasema.

Bw Mudavadi aliwania urais kwa mara ya kwanza mnamo 2013 kwa tiketi ya chama cha UDF, ambapo aliibuka wa nne.

Mnamo 2017, chini ya muungano wa NASA, aliungana na mabwana Raila, Kalonzo na Wetang’ula kukabiliana na Chama cha Jubilee (JP) lakini wakashindwa.