Habari Mseto

Mudavadi, Wetang'ula kutoa mapendekezo kwa BBI mwezi huu wa Februari

February 1st, 2020 2 min read

Na DERICK LUVEGA

KIONGOZI wa Amani National Congress (ANC) Bw Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford-Kenya, Bw Moses Wetang’ula wamesema kuwa watawasilisha mapendekezo yao kwa jopo la Mpango wa Maridhiano (BBI) mwezi huu wa Februari.

Hili liliibuka huku viongozi kutoka Magharibi wakilalama kwamba eneo hilo limetengwa kwenye teuzi za nyadhifa kuu serikalini, licha yao kuunga mkono mpango huo.

Bw Mudavadi alisema kwamba amealikwa na jopo hilo mnamo Februari 11, 2020, akieleza kuwa atatii mwaliko huo na kutoa mapendekezo yake.

Alisema kuwa atakita mapendekezo hayo kulingana na maoni atakayopokea kutoka kwa wananchi.

Kwa upande wake, Bw Wetang’ula alisema kuwa alitoa mapendekezo yake kwenye duru ya kwanza ya jopo hilo kukusanya maoni kutoka kwa wananchi, lakini atafanya hivyo tena kama ishara ya kuonyesha uungwaji mkono wake kwenye mchakato huo.

Hasa, aliiomba Idara ya Sheria kumpa masuala ambayo ingependa yatathminiwe upya ili ayawasilishe kwa niaba yake.

Hii itakuwa mara ya kwanza ambapo Bw Mudavadi atakuwa akiwasilisha mapendekezo yake kwa jopo hilo baada ya kususia mchakato wa kwanza.

Uchumi

Wakati huo, kiongozi huyo alishikilia kuwa Kenya inahitaji kushughulikia hali ya uchumi, kukabili ufisadi, kulainisha idara ya sheria na mchakato wa uchaguzi.

Viongozi hao wamekuwa wakipinga mikutano inayoendelea katika sehemu mbalimbali nchini kuupigia debe mpango huo.

Walikosa kuhudhuria mkutano huo katika eneo la Kisii, lakini wakahudhuria ule uliofanyika mjini Kakamega mnamo Januari 18.

Hii ni licha ya kutangaza awali kwamba hawangehudhuria.

Wakihutubu Jumamosi kwenye mazishi ya Jaji Mstaafu Daniel Aganyanya katika kijiji cha Imusutsu, Kauti ya Vihiga, viongozi hao walisema kwamba ni kupitia jopo hilo tu ambapo masuala yanayowaathiri Wakenya yanaweza kutolewa.

“Tunataka Wakenya wote kufaidika. Kwa sasa, tuna mpango wa BBI. Tunatarajia kwamba mchakato huo utatupa matokeo mazuri,” akasema Bw Mudavadi.

Baadhi ya wale waliohudhuria mazishi hayo ni Jaji Mkuu David Maraga, naibu wake Philomena Mwilu na Mwanasheria Mkuu Paul Kihara.

Alisema kuwa anaunga mkono kuongezwa muda kwa jopo hilo.