Kimataifa

Mugabe kuitwa bungeni kuhusu kutoweka kwa matrilioni

April 11th, 2018 1 min read

Na AFP

HARARE, ZIMBABWE

KAMATI ya wanasheria itamuita rais wa zamani Robert Mugabe bungeni kutoa ushahidi katika kesi ya kutoweka kwa mabilioni ya fedha kutokana na uchimbaji wa madini ya almasi.

Wanasheria hao wanapanga kumhoji Bw Mugabe kuhusu madai yake mnamo 2016 kuwa Zimbabwe ilikuwa imepoteza mapato ya Sh1.5 trilioni kutokana na mauzo ya almasi kutokana na ufisadi.

Mugabe, ambaye uongozi wake ulikejeliwa kwa kuiba faida kutokana na mauzo ya almasi, alifurushwa uongozini na jeshi lililomkabidhi Emmerson Mnangagwa mamlaka.

“Kamati hiyo imekubalina kuwa itamuita Mugabe kutoa ushahidi,” Temba Mliswa, ambaye ni mwanasheria huru anayesimamia kamati ya bunge kuhusu madini na kawi alisema Jumanne.

“Alikuwa rais na tungependa kujua alikokuwa akitoa hesabu ya Sh1.5 trilioni.”

Alisema kuwa tarehe ya kumuita Mugabe bado haijatolewa.

Lakini ni vigumu kujua ikiwa Mugabe, 94, ambaye hajaonekana kwa umma tangu ang’atuliwe, atalazimishwa kuhojiwa na bunge.

Mugabe alitawala taifa hilo kwa miaka 38, akiwa na mamlaka ya kudhibiti bunge kikamilifu, vikosi vya usalama na madini yaliyochimbwa.

Kamati hiyo tayari imewaita mawaziri wa zamani, wakuu wa polisi na maafisa wakuu serikalini kuhusu kashfa hiyo.