Michezo

Muguna kugura Gor

July 24th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NAHODHA wa Gor Mahia, Kenneth Muguna amedokeza nia ya kuagana rasmi na mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) pindi muhula ujao wa uhamisho wa wachezaji utakapofunguliwa.

Kiungo huyo wa zamani wa Western Stima ni miongoni mwa masogora wa haiba kubwa ambao wamekuwa wakihusishwa na uwezekano wa kuvunja uhusiano wao na Gor Mahia mwishoni mwa muhula huu.

Muguna aliwahi kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka wa KPL mnamo 2017 akivalia jezi za Stima. Ni ufanisi huo uliomfanya kuwa andazi moto lililowaniwa na Gor Mahia mwanzoni mwa msimu wa 2018.

“Pengine ni fursa ya kukabiliana na changamoto mpya,” akaandika Muguna kwenye mtandao wake wa Instagram.

Katika mahojiano yake ya awali na Taifa Leo, Muguna aliwahi kukiri kwamba asingechelewa kuikumbatia fursa ya kuingia katika kikosi kingine iwapo ofa nzuri ya kuridhisha ingetokea.

“Siwezi kutabiri ya kesho kwa sababu ningali na kipindi cha miezi 18 katika mkataba wangu wa sasa na Gor Mahia,” aliwahi kusema Muguna huku akisisitiza kwamba kitakachombandua kambini mwa miamba hao ni migogoro ya mara kwa mara pamoja na panda-shuka tele zinazochangiwa na uchechefu wa fedha.

“Hata hivyo, iwapo ofa nzuri itapatikana, basi nitakuwa radhi kuitathmini mradi tu iwasilishwe kwa misingi ya taratibu zilizopo,” akaendelea.

“Kwa sasa ni suala la tusubiri-tuone kwa sababu vikosi vitatu vya haiba kubwa kutoka nje ya Kenya vimefichua maazimio ya kunisajili. Hili la kubishiwa na klabu mbalimbali ni jambo la kawaida kwa mwanasoka yeyote. Na hakuna mchezaji asiyevutiwa na ofa nzuri ya fedha kwa sababu malipo mazuri ni kiini cha hamasa ya kila sogora uwanjani,” akaongeza Muguna ambaye pia amewahi kuvalia jezi za FK Tirana ya Albania kwa kipindi kifupi.

Ingawa kocha Steven Polack wa Gor Mahia amesisitiza kwamba asingependa kabisa kupoteza mchezaji yeyote kambini mwake muhula huu, huenda ikawawia vigumu miamba hao kuwazuilia baadhi ya wanasoka wanaoelekezewa ofa nono kwingineko.

Mbali na Muguna ambaye anamezewa pakubwa na miamba wa Tanzania, Simba SC, masogora wengine wanaotazamiwa kukatiza uhusiano wao na Gor Mahia ni naibu nahodha Joash Onyango, beki Charles Momanyi,  mshambuliaji Nicholas Kipkirui, kipa mzawa wa Tanzania David Mapigano na difenda Dickson Ambundo.

Huku janga la corona na ukosefu wa wadhamini ukizidi kutikisa uthabiti wa kikosi hicho, Gor Mahia wanakodolea jicho hatari ya kulemewa kabisa kifedha kiasi cha kushindwa kumudu mishahara ya wachezaji na maafisa wa benchi ya kiufundi.

Beki Onyango aliyejiunga nao mnamo 2017, amekuwa akimezewa mate na miamba wa soka ya Tanzania, Simba SC ambao pia waliwahi kunyakua mvamizi Meddie Kagere na kiungo Francis Kahata kutoka Gor Mahia. Ambundo anahemewa pakubwa na Yanga SC ambao ni watani wa tangu jadi wa Simba katika Ligi Kuu ya Tanzania.

Kwa upande wake, Mapigano ameapa kutorudi Kenya kuvalia tena jezi za Gor Mahia iwapo mabingwa hao mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) hawatamlipa malimbikizi yote ya mshahara na marupurupu yake.