Habari

Mugure anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mkewe na wanawe wawili anyimwa dhamana

February 21st, 2020 1 min read

Na MERCY MWENDE

MAHAKAMA Kuu mjini Nyeri imemnyima dhamana Peter Mugure anayekabiliwa na mashtaka ya mauaji ya mkewe na watoto wake wawili ikisema anaweza kuvuruga kesi.

Jaji Jairus Ngaah amesema Ijumaa kwamba upande wa mashtaka ukiongozwa na Peter Mailanyi umetoa sababu za kutosha za kumnyima dhamana mshtakiwa.

Kwenye hukumu, jaji amerejelea hati ya kiapo ya afisa aliyechunguza kesi hiyo Reuben Mwaniki ikionyesha kwamba dadake Mugure , Bi Nancy Mugure, alimtembelea mshukiwa wa pili, Collins Pamba katika rumande ya Kerugoya GK.

Jaji amesema ingawa ushahidi uliowasilishwa mahakamani na wakili wa serikali ungali kuthibitishwa mahakamani, upo uwezekano kwamba mshtakiwa anaweza akavuruga kesi iwapo atapewa dhamana.

“Kwenye taarifa iliyoandikishwa na polisi, Pamba anasema mshukiwa ni meja katika kituo cha wanajeshi Laikipia na kwamba alimuahidi kazi ikiwa angenyamaza kuhusu mauaji hayo,” Jaji Ngaah amesema.

Amesema kwa kurejelea cheo ambacho Mugure alishikilia katika kambi ya jeshi, ni vizuri aendelee kuzuiliwa.

Kesi itasikizwa Machi 23, 2019.

Mugure anakabiliwa na mashtaka matatu ya kutekeleza mauaji Oktoba 26, 2019, katika kambi ya Laikipia mjini Nanyuki.

Wahanga wa mauaji hayo walikuwa ni mkewe Joyce Syombua pamoja na wanawe Shanice Maua na Peter Mwaura Jr.

Anadaiwa kutekeleza unyama huo akisaidiwa na watu wengine ambao nao wameshtakiwa.

Upande wa mashtaka una mashahidi 26 ambao inawategemea kutoa ushahidi dhidi ya Mugure.