Habari Mseto

Muhoho abebe mzigo wake, Uhuru adinda kumtetea nduguye

June 28th, 2018 2 min read

WYCLIFFE MUIA na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Alhamisi alisema hatakinga mtu yeyote akiwemo nduguye Muhoho Kenyatta dhidi ya sakata ya kuingiza sukari na bidhaa nyingine haramu nchini.

Akizungumza kwa mara ya kwanza kuhusu msako unaoendelea wa bidhaa haramu nchini, Rais Kenyatta alisema amekuwa kimya kwa sababu ana imani na taasisi zinazokabiliana na suala hilo.

“Nimesikia watu wengine huko nje wakihusisha kakangu na sakata. Kama atapatikana na hatia atakabiliwa na taasisi husika. Kwani kuna shida?” alishangaa rais.

Aliwaonya wanasiasa dhidi ya kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi na kutaka taasisi husika zipewe nafasi ya kufanya kazi.

Alisema ufisadi unawanyima Wakenya huduma muhimu na kuhatarisha mustakabali wa vizazi vijavyo.

Akiongea jana katika Kongamano la Kibiashara la Amerika katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa(UN) eneo la Gigiri, Rais alisema hatakubali taasisi huru kuingiliwa na wanasiasa kwa manufaa yao.

“Sharti tujifunze kuamini taasisi zetu kwamba zitahukumu wenye makosa na kuweka huru wasio na hatia,” alisema Rais Kenyatta.

Kauli ya rais inajiri baada ya baadhi ya viongozi kutoka Rift Valley kuhusisha familia yake na uagizaji wa sukari nchini.

Jumanne, Mbunge wa Aldai, Cornelly Serem alidai kampuni inayomilikiwa na Muhoho Kenyatta ya Protech Investment Limited, iliingiza nchini tani 180,000 za sukari.

Kiongozi wa walio wengi katika Seneti, Kipchumba Murkomen pamoja na Seneta wa Nandi, Samson Cherargei wamekuwa wakipinga agizo la Rais Kenyatta la kuchunguzwa kwa utajiri wa viongozi wakisema agizo hilo halina msingi wa kisheria na kuwa linalenga kuhujumu azma ya Naibu Rais William Ruto kuwa rais 2022.

Akiwajibu jana, Rais Kenyatta aliwataka viongozi haswa walio serikalini wakome kuingiza siasa katika vita dhidi ya ufisadi.

“Nawataka viongozi tafadhali mkomeshe siasa katika suala hili. Kila kiongozi afanye yale yanalenga kuboresha taifa hili,” alisema rais jana.

Hata hivyo, Bw Serem jana alimshutumu Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri kwa kujitenga na orodha ya kampuni zilizoingiza sukari ya magendo nchini, miongoni mwao ikiwa ni ile inayomilikiwa Bw Muhoho.

Mbunge huyo wa chama cha Jubilee alishikilia kuwa madai ya Bw Kiunjuri kwamba jina la kampuni hiyo, Protech Investment Ltd, liliingizwa katika orodha hiyo kimakosa kuwa uwongo.

“Bw Mwenyekiti, kamati hii inafaa kumchukulia hatua Waziri wa Kilimo kwa kukana stakabadhi ambayo yeye mwenyewe ndiye aliyewasilisha mbele yetu mnamo Jumatatu. Ni ishara ya madharau kwa kamati hii kwa Bw Kiunjuri kudai kuwa orodha za kampuni alizowasilisha hapa sio halali,” akasema.

Mnamo Jumanne, Mbunge huyo alidai kuwa Bw Muhoho ni miongoni mwa wafanyabiashara ambao wamekuwa wakiingiza sukari nchini bila kulipia ushuru hivyo kuhujumu sekta ya miwa nchini. Alisema Protech Investment iliorodheshwa nambari 112 katika orodha hiyo iliyotayarishwa na Wizara ya Kilimo.

Lakini mnamo Jumatano, Bw Kiunjuri alikanusha madai hayo akisema nduguye Rais Kenyatta hajawahi kuingiza sukari nchini kutoka nchi za kigeni.

Aliapa kumsaka aliyeingiza jina la kampuni hiyo katika orodha ya kampuni ambazo ziliingiza sukari.

kutoka ng’ambo.