Bambika

Muigai wa Njoroge: Mwanamuziki anayesifika kwa nyimbo za ‘kuilainisha jamii’

March 13th, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

JINA la mwanamuziki Muigai wa Njoroge si jipya miongoni mwa Wakenya, hasa wakazi wa ukanda wa Mlima Kenya.

Ni msanii ambaye amekuwa kwenye tasnia ya muziki wa Injili kwa karibu miongo miwili sasa.

Ijapokuwa mwanamuziki huyo anafahamika kutokana na uimbaji wa nyimbo za Injili, pia amejijengea jina kutokana na na utunzi na uimbaji wa nyimbo za kisiasa.

Tangu aanze safari yake ya muziki katika miaka ya 2000, mwanamuziki huyo amekuwa akitunga mseto wa nyimbo za kisiasa na injili, akishikilia kuwa mwanamuziki ni “macho ya jamii”, hivyo hawezi kunyamaza wakati jamii inapitia changamoto za kiuchumi au kisiasa.

Kwenye safari yake ya muziki, aligeuka kuwa mkosoaji sugu wa serikali ya marais wastaafu Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta.

Amekamatwa mara kadhaa na hata kushtakiwa kwa kutunga nyimbo zilizoonekana kuikosoa serikali au “kuwachochea raia”.

Mnamo 2012, Muigai alikamatwa kutokana na wimbo tata ‘Mwaka wa Nugu’ (Mwaka wa Nyani). Wimbo huo, wakosoaji walisema ulihusiana na tabiri za kisiasa, akilaumiwa kwamba alimaanisha jamii ya Mlimani ingevuna huku wengine wakitupwa nje kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2013.

Kwa msingi huo, wimbo huo ulihusishwa na uchochezi wa kisiasa.  Muigai alishtakiwa pamoja na wanamuziki Kamande wa Kioi na marehemu John De Matthew. Hata hivyo, kesi hiyo iliisha katika hali tatanishi.

Mnamo 2020, Tume ya Kitaifa ya Maridhiano na Utangamano (NCIC) ilimwagiza mwanamuziki huyo kufika mbele yake kutokana na wimbo wenye utata ‘Migunda’ (Mashamba).

Wimbo huo wa kisiasa uliangazia utata ambao umekuwepo nchini kuhusu umiliki wa ardhi.

NCIC ilimtaka kufafanua baadhi ya semi tata kwenye wimbo huo ambao ulikuwa umepata umaarufu mkubwa, hasa katika eneo la Kati.

Kati ya 2020 na 2022, mwanamuziki huyo aligeuka kuwa mkosoaji mkubwa wa serikali ya Bw Kenyatta, huku akitunga nyimbo nyingi za kuikashifu.

Kinaya ni kwamba, aligeuka kuwa muungaji mkono mkubwa wa mrengo wa Kenya Kwanza, uliokuwa ukiongoza na Rais William Ruto (wakati huo akiwa Naibu Rais).

Kwa sasa, mwanamuziki huyo amegonga vichwa vya habari tena kwa kutunga wimbo ambao unawakemea wanawake wenye mienendo isiyo ya uadilifu. Anamulika wanawake wa tabia chwara.

Wimbo huo unaoitwa ‘Nyagacu’ (Mwanamke asiye mwadilifu) umezua gumzo katika majukwaa mbalimbali, hasa katika eneo la Kati, baadhi ya wadadisi wa masuala ya burudani wakisema huenda akapoteza umaarufu wake miongoni mwa mashabiki wake wa kike.

Ikizingatiwa alitoa wimbo huo baada ya kutalikiana na mkewe, Bi Njeeri Muigai, baadhi ya wadadisi wanasema kuwa huenda ukafasiriwa kama njia ya kumchana Bi Njeeri.

“Itamlazimu Bw Muigai kujitokeza na kutoa ufafanuzi kamili kuhusu wimbo huo,” asema Bw John Muchiri, ambaye ni mdadisi wa masuala ya burudani.

Hata hivyo, mwanamuziki huyo anashikilia kuwa “sanaa haina mipaka”.