Makala

Muigizaji Omosh aeneza injili ya ukombozi baada ya kuacha pombe

April 1st, 2024 2 min read

NA WANDERI KAMAU

MNAMO Februari 2021, mwigizaji Joseph Kinuthia, maarufu kama ‘Omosh’, alishangaza Wakenya wengi, alipobubujikwa na machozi akirejelea changamoto za kimaisha alizokuwa akipitia.

Kwenye mahojiano na mwanablogu mmoja, Omosh aliwarai Wakenya kumsaidia kulipa deni la kodi ya nyumba, alilosema lilikuwa karibu Sh100, 000.

“Hali imekuwa ngumu kwangu. Huwa nashindwa niende wapi. Watoto wangu huwa wananiangalia tu, nisijue la kufanya. Kila siku, huwa ninaamka na kutoka nyumbani nisijue ninakoenda,” akasema Omosh, huku akibubujikwa na machozi mbele ya kamera.

Ijapokuwa kilio chake kiligusa maelfu ya mashabiki wake, walioamua kujitolea kumchangia pesa, baadhi walieleza kughadhabishwa na uraibu wake wa matumizi ya vileo.

Naam, Omosh alikuwa amezama kwenye matumizi ya pombe!

Hivyo, baadhi ya mashabiki walisema kwamba hata ikiwa Omosh angechangiwa mamilioni ya pesa, ingekuwa bure ikiwa hakungekuwa na juhudi kumsaidia kuepuka uraibu wa matumizi ya pombe.

Licha ya malalamishi hayo, wasamaria wema walijitokeza na kumsaidia Omosh kununua shamba na kujenga nyumba mpya, ili kuepuka matatizo ya kulipa kodi.

Ingawa mwanzoni mwigizaji huyo alikiri kwamba ilikuwa vigumu kwake kuacha uraibu wa pombe, sasa anaimba wimbo mpya wa ukombozi.

Mwigizaji Joseph Kinuthia ‘Omosh’ akiwa kwenye mojawapo ya hafla za kuihamasisha jamii kuhusu athari za ulevi. PICHA|WANDERI KAMAU

Kwenye mahojiano na Taifa Dijitali mnamo Jumamosi Machi 30, 2024, Omosh alisema uamuzi wake wa kuacha pombe umemletea mafanikio ambayo hakuwahi kudhani angeyapata maishani mwake.

“Bila shaka, hata wewe naamini umeona mabadiliko yangu. Siko vile nilivyokuwa. Mwonekano wangu umeimarika. Ninaweza kucheka. Ninaweza kula chakula bila kufikiria vile nitaenda klabu kununua pombe na vileo vingine hatari,” akasema Omosh.

Hata hivyo, anakiri kuwa safari ya kujikomboa kutoka kwa ulevi haijakuwa rahisi.

Anasema wakati mwingine alikuwa akishawishika kununua pombe au kuvuta sigara, japo anaepuka ushawishi huo alipokumbuka hali aliyokuwa akipitia kabla ya Wakenya kuungana kumsaidia kujenga nyumba.

“Lazima mtu aliye kwenye utumwa wa ulevi afanye uamuzi wa kujikomboa mwenyewe. Nilipelekwa mara kadhaa kwenye vituo vya kusaidia waraibu wa ulevi kuacha matumizi ya vileo, japo juhudi hizo hazikufaulu. Kwa wakati mmoja, wale waliokuwa wakinipeleka walitamauka. Wakaniacha. Ilinilazimu mimi mwenyewe kufanya maamuzi huru ya kujikomboa mwenyewe,” akasema huku akiwa mchangamfu.

Anasema anaunga mkono kikamilifu juhudi zinazoendeshwa na serikali kukabiliana na uuzaji wa pombe haramu nchini.

“Ikiwa ninaweza kujumuishwa kwenye juhudi hizo, inaweza kuwa hatua kubwa katika maisha yangu, kwani itakuwa ni kama kuishukuru jamii kwa juhudi zote ambazo imechukua ili kuninusuru kutoka kwa utumwa wa ulevi,” anasema.

Kwa sasa, Omosh ni balozi wa kutangaza kampuni kadhaa za kibiashara, akisema maisha yake yanafaa kumfungua macho kila mmoja kwamba mtu anaweza kupata nafasi ya pili maishani mwake.

“Ninaimba wimbo wa ukombozi nikimshukuru Mungu kwa kuniokoa kutoka kwa ulevi. Sitarejea Misri tena!” asema.