Mulembe wapigania minofu ya Uhuru

Mulembe wapigania minofu ya Uhuru

Na SHABAN MAKOKHA

ZIARA ya Rais Uhuru Kenyatta katika eneo la Magharibi imegawanya viongozi huku kila mwanasiasa aking’ang’ania ‘minofu’ itakayopelekwa na kiongozi wa nchi.

Wabunge kutoka eneo la Magharibi sasa wanawashutumu magavana wa kaunti tano za Magharibi kwa kukutana na Rais Kenyatta bila kuwashirikisha.

Magavana Wycliffe Oparanya (Kakamega), Wilber Ottichilo (Vihiga), Sospeter Ojaamong (Busia), Patrick Khaemba (Trans Nzoia) na Wycliffe Wangamati (Bungoma) na waziri wa Ugatuzi, Eugene Wamalwa, mnamo Alhamisi, walikutana na Rais Kenyatta jijini Mombasa kupanga ziara hiyo.

Mkutano huo umezua mgawanyiko huku wabunge Ayub Savula (Lugari), Chris Wamalwa (Kiminini) na Titus Khamala (Lurambi) wakidai kuwa magavana hao wamedharau viongozi wengine waliochaguliwa.

Bw Savula alisema kuwa hatua ya magavana hao kukutana na Rais Kenyatta bila kushirikisha kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula pamoja na wabunge kutoka Magharibi ni ishara kwamba viongozi hao wa kaunti wamewadharau.

Mbunge huyo alisema: “Eneo la Magharibi lina changamoto tele ambazo zinafaa kushughulikiwa na viongozi wote.”

Alisema wabunge walifaa kuhudhuria mkutano huo kumweleza Rais Kenyatta miradi ambayo inafaa kupewa kipaumbele. Alisema magavana hao wanataka kutumia miradi itakayozinduliwa na Rais Kenyatta kujitafutia umaarufu wa kisiasa.

“Magavana hawaelewi changamoto zote zinazokumba watu wetu. Kila kiongozi alifaa kuhudhuria mkutano huo ili tueleze changamoto zetu,” akasema Bw Savula.

Kulingana na mbunge wa Lugari, kiongozi wa ODM Raila Odinga ndiye amepanga ziara hiyo ya Rais Kenyatta katika eneo la Magharibi na yeye ndiye anataka Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula watengwe.

“Bw Odinga anataka kutumia magavana kupanga ziara hiyo ili aandamane na Rais Kenyatta atakapozuru eneo la Magharibi. Hatutaruhusu Bw Odinga kutupangia mkutano wetu,” akadai.

Alisema kuwa Rais Kenyatta hana budi kupitia kwa Bw Mudavadi kabla ya kupanga ziara yake katika eneo la Magaharibi.

Bw Wamalwa alisema kuwa magavana waliokutana na Rais Kenyatta wanataka kujijenga kisiasa kwa kudunisha viongozi wengine waliochaguliwa.

Bw Khamala alisema kuwa viongozi wa Magharibi watasusia ziara hiyo ya kiongozi wa nchi iwapo hatahusisha Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula katika mipango.

“Hakutakuwa na haja ya kwenda kumlaki Rais Kenyatta ikiwa Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula, ambao wana usemi mkubwa wa kisiasa katika eneo hili, watatengwa katika maandalizi ya ziara hiyo,” akasema Bw Khamala.

Alisema kwamba Rais Kenyatta alipozuru eneo la Nyanza na Ukambani, alikutana na vigogo wa kisiasa wa maeneo hayo kabla ya kwenda.

Rais Kenyatta anatarajiwa kuzuru eneo la Magharibi wiki ijayo ambapo atazindua miradi mbalimbali ya maendeleo.

Bw Oparanya, hata hivyo, alisema magavana walikutana na Rais Kenyatta ili kumsihi kuzuru eneo la Magharibi.

“Hatuwezi kualika viongozi wote kutoka Magharibi kwenda kumlaki Rais atakapozuru eneo hilo. Kwa sababu Rais Kenyatta tayari amekubali kuzuru Magharibi sasa tutaalika viongozi wote ili tufanye maandalizi,” akasema.

Kulingana na Bw Oparanya, Rais Kenyatta atazuru eneo la Magharibi kwa siku tatu na ajenda kuu itakuwa kufufua viwanda vilivyoporomoka kati ya miradi mingineyo ya maendeleo.

“Tulimsihi kufufua viwanda vya sukari vilivyoporomoka vya Mumias, Nzoia na kiwanda cha karatasi cha PanPaper,” akasema kiongozi wa Kakamega.

You can share this post!

Utalii wapigwa jeki Lufthansa ikizindua safari

Watekaji nyara wamnyaka mzee aliyewapelekea Sh7m