Mulembe wapongeza Mudavadi, Weta’

Mulembe wapongeza Mudavadi, Weta’

NA BRIAN OJAMAA

WAKAZI na viongozi kutoka eneo la Magharibi wamepongeza kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya, Moses Wetang’ula kwa kuungana na Naibu wa Rais William Ruto.

Walisema hatua hiyo itawezesha jamii ya Mulembe kuingia serikalini Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu baada ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Wakazi na viongozi hao waliokuwa wakihutubia wanahabari mjini Bungoma, walisema kuwa wapigakura wa eneo hilo wamechoka kumuunga mkono kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye hajaonyesha shukrani.

“Muungano wa ANC na United Democratic Alliance (UDA) utasababisha Bw Odinga kukosa kura katika eneo la Magharibi,” akasema Bw Isack Wanjekeche, mwanaharakati wa kisiasa.

Kulingana na Bw Wanjekeche, Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wanadhibiti siasa za Magharibi hivyo itakuwa rahisi kwao kujizolea kura nyingi.

Anasema kuwa chama cha DAP-K kinachohusishwa na waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, kimepata pigo.

“Muungano wa Ford Kenya, ANC na UDA ni pigo kwa chama cha DAP-K ambacho sasa kitakuwa na wakati mgumu kushawishi wakazi wa Magharibi kuunga mkono vuguvugu la Azimio la Umoja lake Bw Odinga,” akasema.

Bw Wanjekeche alisema kuwa Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula walimtoroka Bw Odinga kwa sababu ‘haaminiki’.

Mwanasiasa anayemezea mate udiwani wa Wadi ya Cheptais eneobunge la Mlima Elgon, Amos Chemabus, alisema kuwa muungano wa Bw Mudavadi na Dkt Ruto utasaidia kudumisha utulivu wa kisiasa nchini.

  • Tags

You can share this post!

Ushirikiano wa Mudavadi, Ruto waibua tumbojoto huku...

TAHARIRI: Tubadili mtindo wa kudumisha amani uchaguzi...

T L