Michezo

Mulukurwa pazuri kuteuliwa kocha mkuu wa Nzoia Sugar

November 12th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Nzoia Sugar FC kimeanza mchakato wa kutafuta mkufunzi mpya kwa minajili ya kampeni za Ligi Kuu ya Kenya (FKFPL) msimu ujao wa 2020-21.

Klabu hiyo iliwahoji wakufunzi watano waliotuma maombi ya kazi kambini mwao mnamo Novemba 9, 2020 katika afisi za kampuni ya sukari ya Nzoia Sugar, Bungoma.

Watano hao walihojiwa na Kamati Kuu ya kikosi chini ya uongozi wa mwenyekiti wa klabu, Evans Kadenge. Mbali na Sylvester Mulukurwa ambaye kwa sasa ni kocha mshikilizi wa kikosi Nzoia Sugar, wengine waliohojiwa ni Leonard Odipo, James Nandwa, John Nams na Ibrahim Shikanda ambaye pia amewahi kuwa kocha msaidizi kambini mwa Bandari FC.

Odipo amewahi kudhibiti mikoba ya Nairobi Stima naye Nandwa amewahi kuwa mkufunzi mkuu wa kikosi cha Thika United.

Wadhifa wa mkufunzi mkuu kambini mwa Nzoia ilisalia wazi mnamo Machi 2020 baada ya mkufunzi Collins ‘Korea’ Omondi kutimuliwa kwa sababu ya matokeo duni ya kikosi hicho kilichoambulia nafasi ya 15 kwa alama 13 kwenye jedwali la vikosi 18 vya Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2019-20.

Baada ya Omondi kufutwa kazi, Mulukurwa ambaye anapigiwa upatu kuwa mkufunzi mkuu mpya wa Nzoia Sugar, aliteuliwa kuwa kocha mshikilizi.

“Nina wingi wa matumaini kwamba nitapokezwa mikoba ya Nzoia Sugar baada ya kufanyiwa mahojiano mnamo Novemba 9. Sasa nasubiri matokeo ambayo usimamizi umesema yatatolewa rasmi hivi karibuni,” akasema kocha huyo.

Nzoia Sugar ni miongoni mwa vikosi vya Ligi Kuu ya Kenya zilivyojishughulisha zaidi sokoni muhula huu kwa kusajili jumla ya wanasoka 12 kadri wanavyozidi kujisuka upya kwa minajili ya kampeni za msimu ujao wa 2020-21 katika FKFPL.

Mbali na Daniel Kakai aliyetua Nzoia Sugar kwa mkopo kutoka AFC Leopards, wachezaji wengine ambao walirasimisha uhamisho wao hadi kambini mwa wanasukari hao ni walinzi Gabriel Wandera na Elivis Ronack Otieno kutoka Tusker na Gor Mahia mtawalia.

Mwenyekiti wa Nzoia Sugar, Evance Kadenge, pia amethibitisha kwamba wachezaji tisa waliagana rasmi na kikosi hicho muhula huu.

“Tulikatiza uhusiano na wachezaji ambao benchi ya kiufundi ilihisi kwamba hawakuridhisha wala kufikia kiwango cha matarajio ya usimamizi kufikia mwisho wa msimu wa 2019-20,” akasema.

Kwa mujibu wa Kadenge, Nzoia Sugar bado wana azma ya kuvunja ndoa na wanasoka kadhaa katika muhula mfupi ujao wa uhamisho wa wachezaji wa kivumbi cha FKFPL.

“Lengo letu ni kusalia na idadi ya wachezaji ambao tunaweza kumudu mahitaji yao kifedha. Iwapo kuna yeyote atakayetaka kuagana nasi, basi yuko radhi kufanya hivyo. Hatutamzuia mchezaji yeyote kuondoka kwa lengo la kutafuta hifadhi mpya, ambayo kulingana naye, itampigisha hatua kubwa zaidi kitaaluma,” akaongeza Kadenge.

Miongoni mwa sajili wapya wa Nzoia Sugar kufikia sasa ni kipa Mustapha Oduor, Moses Mudavadi na Cliff Kasuti — wote kutoka Bandari FC. Wengine ni mvamizi Felix Oluoch (Posta Rangers), kiungo Eric Mango (KCB) na Titus Kapchanga (St Anthony’s Kitale). Beki Kevin Maliachi alijiunga na wanasukari hao baada ya kuagana na APS Bomet inayoshiriki Ligi ya Kitaifa ya Supa (NSL).

Hadi walipoingia katika sajili rasmi ya Nzoia Sugar, Brian Wanyonyi na Jeremiah Juma hawakuwa na klabu.

Mohammed Nigol, Robert Abonga, Chris Wesamba, Masoud Juma, Abraham Kipkosgei, Faraj Kibali, Boris Kwezi, Jeremiah Wanjala na Vincent Odongo aliyeyoyomea Kariobangi Sharks ni miongoni mwa wachezaji ambao walikatiza uhusiano na Nzoia Sugar.

“Tumeanza mchakato wa kumwajiri mkufunzi mpya ambaye ana leseni ya daraja la C kutoka kwa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF). Hayo ndiyo masharti kwa kocha yeyote anayedhibiti mikoba ya kikosi cha Ligi Kuu ya Kenya,” akasema Kadenge kwa kufichua kwamba walipokea maombi ya kazi kutoka kwa wakufunzi 10 ila wakatia watano pekee kwenye orodha fupi ya mwisho ya wale waliohojiwa.

“Idara yetu inayoshughulikia masuala ya ajira inatazamiwa kutangaza kocha mpya hivi karibuni baada ya watano kati ya 10 waliotuma maombi ya kazi kuhojiwa,” akasisitiza Kadenge aliyepokezwa uenyekiti wa Nzoia mnamo Februari 2020 baada ya kuondoka kwa Yappets Mokua.