Dondoo

Mume achomoa upanga mazishi ya mke

May 5th, 2019 1 min read

NA TITUS OMINDE

Kifinko, Kakamega

Kulitokea kizaazaa kwenye sherehe ya mazishi kijijini hapa mwanamume aliyefiwa na mkewe alipotoroka akibeba upanga baada ya kulaumiwa na wakwe zake kwa kuwa mraibu wa bangi hata wakati wa mazishi.

“Huyu mwanamume amepotelea katika uvutaji bangi, huenda tabia hii ndio imechangia kifo cha dada yetu, wakati tunapanga mazishi yeye hutorokea vichakani kuvuta bangi, sijui huyu ni mume wa aina gani,” alisema mama mkwe akihutubia waombolezaji.

Jamaa wa marehemu waliambia waombolezaji kuwa mwanaume alikuwa akiondoka mara mwa mara kwenda kuvuta bangi ibada ikiendelea.

Kulingana nao, tabia hiyo ilikuwa kero kwa dada yao jambo ambalo lilimsababishia msukumo wa damu na magonjwa mengine.

Mwanamume huyo alidaiwa pia wakati mmoja aliteketeza nyumba yake baada ya kuvuta bangi na kudai kuwa marehemu alikuwa amebadilika na kuwa jini.

Shutuma zilipozidi wakati wa ibada jamaa aliamua kutoroka huku akiwa amebeba panga ili kumvamia yeyote ambaye angethubutu kumrudisha katika ibada ya mazishi ya marehemu mke wake.

Polo huyo alitokomea huku akiwaaacha waombolezaji wakiwa wameshangaa.

Juhudi za kumshawishi kuvumilia hadi ibada iishe ziliambulia patupu kwani hakusikia la mtu yeyote.

Inandaiwa kuwa mwanume huyo alirejea baada ya mazishi ambapo aliamrisha wakwe kuondoka haraka bomani mwake hasa baada ya kumharibia jina wakati wa ibada.

“Sitaki kuona mtu yeyote katika boma la mvuta bangi, mmeniharibia jina katika ibada, sasa shikeni safari ya kurudi kwenu la sivyo mtajua huu ni upanga wenye makali,” alisema polo huyo huku akibusu upanga wenye makali aliokuwa ameshika mkononi.

Ilibidi ndugu na jamaa wa marehemu kukimbilia usalama wao kutoka boma hilo.