Shangazi Akujibu

Mume hujisaidia kitandani, nimechoka kufua shuka kila siku!

April 25th, 2024 1 min read

Shangazi,

Mume wangu wa miaka 10 na nampenda sana. Tatizo ni kwamba katika muda huu wote amekuwa akikojoa kitandani tangu tuoane. Nimekuwa nikifua shiti kila siku!

Tatizo la kukojoa kitandani hasa kwa watu waliokomaa kiumri, ni la kiafya. Je uko tayari kumtema mtu kwa sababu ya jambo asiloweza kuzuia, hasa ikiwa mambo mengine anatimiza?

Nimegundua mpenzi analipiwa kodi na shuga dadi!

Nimekuwa nikichumbiana na huyu binti kwa miezi na wakati mwingine nimekuwa nikienda kulala kwake. Wikendi iliyopita tulienda kwake. Lakini usiku wa manane, tuliamshwa kwa vishindo na baba sukari anayelipa nyumba.

Ni makosa sana kwenda kulala katika nyumba usiyolipa. Pili, kama bado hamjaoana, si wako, kumaanisha kwamba kuna wengine. Sasa wewe amua.

Ataka picha ya marehemu mkewe ibaki kuwa ukutani

Nimeolewa na mume wangu kwa miaka miwili. Tulioana baada ya mkewe kufa na tukakubaliana kuunganisha familia zetu. Hata hivyo, anasisitiza picha ya marehemu mkewe iendelee kuning’inia sebuleni.

Hilo ni jambo zito. Si rahisi kumpoteza mwenza, lakini pia si haki kwako kuendelea kuishi maisha hivi. Zungumza naye, lakini unapofanya hivyo, jaribu kumwambia kwa upole kwani pengine bado anamuomboleza marehemu mkewe.

Ana mke tasa, anasukuma niolewe nimzalie watoto!

Hujambo shangazi? Nimekuwa katika uhusiano na huyu kaka ambaye ni mume wa mtu. Lakini mkewe wa kwanza ni tasa. Anataka kunioa ili nimzalie. Nikubali?

Sijambo. Swali langu ni je, unajuaje si huyo mwanamume mwenye tatizo? Hata hivyo, ikiwa mmeamua kufanya hivyo, wekeni mambo wazi hasa mbele ya mkewe!