MUME KIGONGO: ‘Magonjwa ya wanawake’ ambayo yanaumiza wanaume kimya kimya

MUME KIGONGO: ‘Magonjwa ya wanawake’ ambayo yanaumiza wanaume kimya kimya

NA LEONARD ONYANGO

KUTOKANA na tofauti ya kimaumbile, baadhi ya magonjwa hulemea jinsia moja kuliko nyingine.

Kwa mfano, baadhi ya magonjwa kama vile kansa ya matiti, hulemea wanawake zaidi kuliko wanaume. Hali hiyo hufanya wanaume kuyapuuza wakidhani ni ‘magonjwa ya wanawake’.

Baadhi ya maradhi yanayochukuliwa kuwa ‘magonjwa ya wanawake’ pia huathiri wanaume japo idadi ndogo ni:

•Udhaifu wa mifupa: Ugonjwa huu ambao pia unajulikana kama osteoporosis husababisha mifupa kuwa dhaifu na mwathiriwa huweza kuvunjika miguu kwa urahisi. Huathiri idadi kubwa ya wanawake haswa wa umri wa miaka 65 na zaidi. Lakini wanaume pia wanaweza kukumbwa nao. Ugonjwa huu hauna dalili ila unaweza kugunduliwa baada ya vipimo. Ukosefu wa vitamini D mwilini na matibabu ya Kansa yanaweza kuchangia mifupa kuwa dhaifu.

•Kansa ya matiti: Japo idadi kubwa ya wanawake ndio huathirika, wanaume pia wanaweza kuugua. Kansa ya matiti miongoni mwa wanaume inaweza kugunduliwa kwa kugusa matiti ili kubaini ikiwa kuna uvimbe.

•Maambukizi ya kibofu cha mkojo: Matatizo ya kibofu cha mkojo (Bladder infections) mara nyingi hushuhudiwa miongoni mwa wanawake. Lakini wanaume wanaweza kupata shida hiyo pia haswa walio na matatizo ya figo. Dalili za ugonjwa huo ni kukojoa mara kwa mara na damu kwenye mkojo.

•‘Lupus’: Asilimia 90 ya wagonjwa wa Lupus huwa wanawake. Lakini ugonjwa huo ambao hushambulia viungo vya mwili unaweza kuathiri wanaume pia. Dalili zake kwa wanaume ni kufura kwa vifundo vya mwili, kudhoofika kwa misuli, uchovu, kufura kwa miguu kati ya nyinginezo.

•‘Human Papillomavirus (HPV)’: Virusi vya HPV huathiri idadi kubwa ya wanawake kwani huchangia kwa kiasi kikubwa kwa kansa ya lango la uzazi. Lakini vinaweza kuathiri wanaume pia na kusababisha kansa katika sehemu nyeti.

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Ugonjwa wa MS hauna tiba lakini waweza...

JIJUE DADA: Kutokwa damu nyingi wakati wa hedhi na kwa muda...

T L