MUME KIGONGO: Wataalamu sasa wahusisha ugumba na kansa ya matiti kwa wanaume

MUME KIGONGO: Wataalamu sasa wahusisha ugumba na kansa ya matiti kwa wanaume

NA LEONARD ONYANGO

WANAUME wasio na uwezo wa kutungisha mimba wako katika hatari ya kukabiliwa na tatizo la kansa ya matiti, utafiti umedai.

Utafiti mkubwa uliofanywa nchini Uingereza na Taasisi ya Kutafiti Kansa (ICR), ulibaini kuwa kansa ya matiti ilipendelea zaidi wanaume wasio na uwezo wa kutungisha mimba ila bado haijulikani kinachosababisha hali hiyo.

Ripoti ya utafiti huo ilichapishwa katika jarida la Breast Cancer Research.

Kansa ya matiti huwapata wanaume japo kwa kiwango cha chini ikilinganishwa na wanawake.Wanasayansi wangali hawafahamu kinachosababisha kansa hiyo kwa wanaume.

Dkt Sitna Mwanzi, mtaalamu wa tiba ya kansa jijini Nairobi anasema kuwa kwa kila wanawake 100 walio na kansa ya matiti humu nchini, mwanamume mmoja ana maradhi hayo.

Wataalamu katika Chuo Kikuu cha Queen, Uingereza, na Chuo Kikuu cha Sapienza cha Italia wanaendelea na utafiti kubaini kinachosababisha kansa hii kwa wanaume.

“Matokeo ya utafiti wetu yanaonyesha kuwa kuna uhusiano kati ya ugumba na ongezeko la kansa ya matiti miongoni mwa wanaume. Kinachosababisha hali hiyo hakijulikani na kuna haja ya utafiti zaidi ili kubaini uhusiano uliopo,” inasema ripoti hiyo ya wataalamu wa ICR.

Watafiti wa ICR walihusisha wanaume 1,998 waliopatikana na kansa katika utafiti huo nchini Uingereza. Wanaume hao walifuatiliwa kwa kipindi cha miaka 12.

Aidha wanaume hao waliulizwa ikiwa wamewahi kuwa na mpenzi au wamewahi kumpachika mwanamke mimba.

Ilibainika kuwa wengi wao hawakuwa na wapenzi kutokana na ukosefu wa nguvu za kiume na wengine hawakuwa wamewahi kumpachika mwanamke mimba.

You can share this post!

Gavana Lenku aitaka serikali kuu kutoa msaada wa chakula

Ruto atarajiwa Pwani wandani wakizozana

T L