MUME KIGONGO: Wazee wanywe maji hata wasipohisi kiu – watafiti

MUME KIGONGO: Wazee wanywe maji hata wasipohisi kiu – watafiti

NA CECIL ODONGO

WAZEE wanahitaji kunywa maji mara kwa mara hata wasipohisi kiu kuliko vijana, utafiti umebaini.

Japo kunywa maji mara kwa mara ni hitaji la kiafya kwa watu wa umri wowote ule, watafiti wanasema, kwa wazee ni muhimu zaidi kwa sababu hawahisi kiu ikilinganishwa na walipokuwa ujanani.

Wakati ambapo kuna joto jingi, homoni inayofahamika kama hypothalamus husababisha ngozi kutoa jasho na kusababisha mtu ahisi kiu kisha kunywa maji ya kusawazisha yale ambayo yamepotea.

Watafiti wa Chuo Kikuu cha Ottawa, Canada walipata kuwa wazee huwa hawahisi kiu kama watu wa umri mdogo au vijana kwa sababu mwili hauwezi kusawazisha kiwango cha maji na chumvi iliyoko kwenye damu mwilini.

Hii ni kinyume na vijana ambapo mwili hutambua haraka kiwango cha chumvi kinapopanda kwenye damu kisha ngozi huanza kutoa jasho na kusababisha mtu ahisi kiu haraka.

Pia, utafiti huo uligundua kuwa ukosefu wa maji mwilini mwa wakongwe hausababishi kupanda kwa joto jinsi ambavyo ipo kwa vijana au katika hali ya kawaida.

Ingawa hili ni jambo zuri Kisayansi, kwa kiasi fulani lina athari zake kwa sababu mwili hukosa kutoa dalili kuwa mtu amepoteza maji mengi yanayostahili kusawazishwa ili kupunguza joto.

Aidha, wazee huandamwa na maradhi mbalimbali kama kisukari ambayo husababisha mwili wao kushindwa kudhibiti kiwango cha joto mwilini.

Athari ya magonjwa hayo hufanya wasihisi kiu na mwili wao huishia kukosa maji, hali ambayo pia husababisha uchovu na maumivu ya misuli.

  • Tags

You can share this post!

Vihiga Queens na Nakuru City Queens wapigana vita vikali...

BENSON MATHEKA: Inashangaza hongo kutozwa hadharani na...

T L