Dondoo

Mume mchafu afungiwa bafuni aoge

June 29th, 2019 1 min read

Na JOHN MUSYOKI

MLOLONGO, MACHAKOS

KIOJA kilishuhudiwa kwenye ploti moja mjini hapa mwanadada alipomfungia kalameni ndani ya bafu akimtaka aoge mwili mzima.

Kulingana na penyenye za mtaani, jamaa alikuwa amesusia kuoga kwa muda mrefu hadi mke wake akakasirika.

Siku ya kioja jamaa aliporejea nyumbani kutoka shughuli zake za kila siku, aliitwa na mke wake bafuni huku akimdanganya mfereji ulikuwa umeharibika.Yadaiwa jamaa alipokaribia bafuni mke wake alimsukuma ndani na kufunga mlango kwa kufuli.

“Ulidhani wewe ni mwerevu. Ujanja wa nyani huishia jangwani. Nimekuwekea maji, taulo na sabuni. Mara utakapooga nitakufungulia mlango. Umekuwa ukihepa kuoga kwa muda mrefu,” demu alimwambia jamaa.

Jamaa alilalamika na kuanza kupiga mlango wa bafu kwa nguvu. Wapangaji waliokuwa karibu walishangazwa na kitendo hicho lakini mke wake alishikilia msimamo wake.

“Msishangae wala msivunje mlango. Ni mume wangu ambaye yumo humo ndani. Namtaka aoge kwanza. Amekuwa akisusia kuoga na leo hii nitamfunza adabu,” demu alisikika akiwaambia wapangaji.

Wapangaji walishangaa huku wengine wakiangua vicheko kufuatia hatua ya mwanadada huyo. Yasemekana jamaa hakuwa na jingine ila kuvua mavazi yake na kuoga.

Mke alipothibitisha kwamba jamaa alikuwa ameoga alimfungulia mlango.

“Nadhani leo umeshika adabu, utakuwa ukioga mara mbili kila siku,” demu alimwambia jamaa.

Inasemekana jamaa alitulia tuli bila kusema chochote kwa sababu alikuwa ameaibishwa na mke wake.

Kulingana na mdokezi, tangu siku hiyo jamaa amekuwa akionekana akiingia bafuni kila siku kuoga na kubadilisha mavazi jambo ambalo lilikuwa mwiko kwake kabla ya mkewe kuchukua hatua.