Habari

Mume, mke wafikishwa mahakamani wakidaiwa kuua mtoto wao Murang'a

June 4th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

MWANAMUME na mkewe katika Kaunti ya Murang’a Jumatatu walifikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kuua mtoto wao wa kike ambaye hadi wakati akikumbana na mauti alikuwa na umri wa miaka miwili na nusu.

Stephen Kamau pamoja na mkewe, Bi Mildred Muasya, walifikishwa mbele ya hakimu Sheila Nyagah kujibu shtaka hilo.

Mahakama hiyo ya Murang’a ilikuwa imefurika, hamu ya kujua hasa ukatili wanaohusishwa nao ulitokana na kishawishi gani.

Hata hivyo, wawili hao hawakupewa fursa ya kujibu shtaka hilo kwa kuwa wapelelezi hawakuwa wamemaliza uchunguzi.

Upande wa mashtaka katika hali hiyo uliomba mahakama iwaruhusu

kuwazuilia wawili hao katika seli za kituo cha polisi cha Murang’a kwa

siku 14 ili waimarishe uchunguzi wa kuandaa mashtaka thabiti.

Hakimu Sheila Nyaga akitoa mwelekeo kuhusu kesi ya mume na mkewe waliofikishwa mbele yake kujibu shtaka la kuua binti yao aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu na kutupa mwili wake ndani ya mto. Picha/ Mwangi Muiruri

Akiwapa ruhusa hiyo, hakimu Nyaga alisema kuwa alikubaliana na kitengo cha uchunguzi wa jinai kuwa “shtaka hili linahitaji uchunguzi wa kina” na akawapa idhini hiyo ya kuwazuilia wawili hao hadi Juni 17, 2019, ambapo kesi hiyo itatajwa.

Wawili hao walionekana kushtuka na kujawa na taharuki mbele ya mahakama hiyo.

Ni wakazi wa kijiji cha Kabui katika wadi ya Gaturi iliyoko kaunti ndogo ya Kiharu.

Wanadaiwa kuwa walimuua mtoto huyo wao kati ya Jumamosi na Jumapili na kisha kupakia mwili katika gunia na kuutupa ndani ya mto wa Mathioya.

Mabaki hayo yalipatikana Jumapili na ambapo wawili hao walikamatwa na kuhusishwa na mauaji hayo, ghadhabu zikitanda katika kijiji chao kiasi kwamba kulikuwa na njama ya kuwavamia na kuwaadhibu kwa haki ya kitutu.

Lakini maafisa wa kiusalama walipata dokezi na kando na kuwakamata kwa nia ya kuwachunguza zaidi na kuwashtaki, wakafika eneo hilo na kuwanusuru.

Sasa, harakati za kuwaandalia mashtaka ndipo upande wa mashtaka utaelezea dunia ushahidi wa kuwahusisha na mauaji hayo, uwasilishe mashahidi na hatimaye utoe sababu hasa za ukatili huo kutekelezewa mtoto na wazazi wake, mamake mzazi akiwemo licha ya msemo kuwa ajuaye uchungu wa mwana ni mzazi.

Hatia

Iwapo watapatikana na hatia ya kutekeleza mauaji hayo, hukumu ni ya kifo au kufungwa maisha gerezani, ikiwa ni kifungo wawe wametenganishwa wala sio wafungwe wakiwa pamoja kuendelea kuishi kama mume na mke.

Kwa sasa, katiba ya Kenya imepiga marufuku kuuawa kwa wafungwa licha ya kuwa sheria za nchi bado zinatoa hukumu hiyo.

Katika msingi huo, hukumu ya kifo nchini ni sawa na kifungo cha maisha gerezani.