Habari Mseto

Mume, mke wakamatwa kuhusiana na mauaji ya mwanamke katika zogo la kimapenzi

May 30th, 2024 1 min read

Na VICTOR RABALLA

POLISI wanazuilia mwanamume na mwanamke kwa kuhusika na mauaji ya mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 22.

Kamanda wa Polisi wa Kisumu ya Kati, Peter Mulai, alisema marehemu ambaye anatambuliwa kama Vincy Juma, aliaga dunia kutokana na majeraha aliyoyapata baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya pili.

Tukio hilo lilifanyika katika mtaa wa Lolwe viungani mwa jiji la Kisumu.

Kwa mujibu wa majirani, mwanamke aliyeuawa alifika nyumbani kwa mpenziwe wake wa zamani na akampata wakiwa na mwanamke mwingine. Watatu hao walivurugana na marehemu akarushwa kutoka ghorofa ya pili.

Alipata majeraha ya kichwa na akaloa damu. Mwanaume huyo, 30, alipoona hali yake ilikuwa hatarini, alimpelekea haraka hadi hospitalini ambapo ilithibitishwa alikuwa amefariki.

Bw Mulai alisema kuwa makachero bado hawajabaini iwapo alisukumwa kutoka ghorofa ya pili.

Mwanaume huyo na mpenziwe wanaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central na watafikishwa kortini baada ya uchunguzi kukamilika.