Habari Mseto

Mume wa wake wawili walioshtakiwa kumiliki bunduki pia akabiliwa kisheria

February 13th, 2018 2 min read

Mume wa wanawake wawili Bw Ibrahim Gedi Abdile akiwa kizimbani katika mahakama ya Nairobi aliposhtakiwa kumiliki silaha kinyume cha sheria Februari 12, 2018. Picha/ Richard Munguti

Na RICHARD MUNGUTI

Kwa Muhtasari:

  • Ibrahim Gedi Abdile alijisalamisha kwa maafisa wa polisi kaunti ya Wajir baada ya kufahamishwa wake zake
  • Ajieteta kuwa yeye ni mfugaji. Bunduki ilikuwa ya kujikinga  pamoja na wake zake, watoto na mifugo!
  • Makosa ya wanawake hao ni kuolewa na mume anayeshukiwa kuwa mwanachama wa kundi haramu la Al Shabaab
  • Kiongozi wa mashtaka alipinga wakiachiliwa kwa dhamana akisema serikali inahofia watatoroka

MUME wa wanawake wawili mmoja wao nyanya wa miaka 70 walioshtakiwa wiki mbili zilizopita kwa kumiliki bunduki aina ya AK47, alipotorokea nchini Somalia asikamatwe, alishtakiwa Jumatatu.

Bw Ibrahim Gedi Abdile alijisalamisha kwa maafisa wa polisi kaunti ya Wajir baada ya kufahamishwa wake wake wawili walitiwa nguvuni na kusafirishwa jijini Nairobi.

“Mshtakiwa alijisalamisha kwa polisi na kuwapa bunduki iliyokuwa ikisakwa,” kiongozi wa mashtaka Bi Cynthia Opiyo alimweleza hakimu mwandamizi Bw Kennedy Cheruiyot

Mshtakiwa alimweleza hakimu: “Mimi ni mfugaji. Bunduki hii ilikuwa ya kujikinga  mimi, wake wangu , watoto na mifugo.”

Abdile alikanusha shtaka na wakili David Ayuo aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Alidaiwa alimiliki bunduki kinyume cha sheria katika kijiji cha Bula Elmi kilicho kaunti ndogo ya  Wajir Mashariki mnamo Januari 24, 2018.

 

Risasi

Pia alishtakiwa kwa kumiliki raudi 80 za risasi. Aliachiliwa kwa dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu.

Katika kesi iliyowakabili wake zake wawili, wakili Dunstan Omari alimweleza hakimu mkazi Bi Hellen Onkwani, “ wanawake hawa hawana makosa. Makosa yao ni kuolewa na mume anayeshukiwa kuwa mwanachama wa kundi haramu la Al Shabaab.”

Wanawake hawa walishtakiwa kumiliki bunduki aina ya AK47. Mahakama iliwaachilia huru wiki mbili zilizopita baada ya wakili wao kuishawishi kuwa makosa yao ni kuolewa na mwanaume anayeshukiwa na polisi kwa tuhuma za kuwa na uhusiano magaidi wa Al Shabaab. Picha/ Richard Munguti

Bw  Omari alimsihi Bi Onkwani awaachilie wanawake Bi Nurea Adhan Jimale (70) na Halima Sheikh Abdullahi hao kwa dhamana ili “warudie watoto wao kwa vile mume wao  alitorokea Somalia na watoto wako peke yao nyumbani.”

“Wanawawake hawa hawana hatia. Makosa yao ni kuolewa na mwanaume anayeshukiwa na polisi kwa tuhuma za kuwa na uhusiano magaidi wa Al Shabaab.”

Bw Omari alimweleza hakimu washukiwa walisafirishwa kutoka kaunti ya Wajir baada ya hakimu katika korti ya Wajir kuamuru waachiliwe kwa dhamana.

 

Wanateswa bure

“Wanawake hawa wanateswa bure. Waliachiliwa na mahakama ya Wajir kisha wakakamatwa tena na kusafirishwa hadi Nairobi kuzuiliwa.

Polisi wanawadhulumu kwa vile wanatoka eneo la mpaka wa Kenya na Somalia. Mume wao anadaiwa alitorokea nchi jirani. Washtakiwa hawa wanadhulumiwa kwa vile wameolewa na mtoro,” alisema wakili Omari.

Bw Omari alisema alikuwa amepeleka ombi katika mahakama  kuu na Jaji Luka Kimaru akaamuru kesi itajwe Feburuari 5, 2018.

Kiongozi wa mashtaka alipinga wakiachiliwa kwa dhamana akisema “serikali inahofia watatoroka.”

Bi Onkwani aliwaachilia wanawake hao kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu.

Kesi dhidi ya wanawake hao na mume wao itasikizwa Machi 8, 2018.