Bambika

Mumewe Christina Shusho aumia ndoa kuvunjika

May 6th, 2024 2 min read

Na SINDA MATIKO

MUMEWE mwanamuziki staa wa nyimbo za injili kutoka bongo Christina Shusho amerusha jiwe gizani kufuatia kauli ya mkewe kuhusu sababu zake za kuondoka kwenye ndoa yao.

Mwezi uliopita, Christina alidai kuwa alivunja ndoa yake ili aweze kumtumikia Mungu.

“Acha nisemi hili kwa roho safi, mimi sijawahi kuwa feki sijui kusema uwongo na naomba watakaofuatilia hili waamini ndio mimi. Ukweli ni kwamba ni mwito tu wa kumtumikia Mungu, hamna kitu kingine tofauti na hilo. Mwito ambao Mungu amenipa kipindi hiki, haiwezi kukaa pale nilipokuwa kwa hiyo lazima nitoke ili nikaitimize. Na sio kwamba nataka kuwa pasta Shusho, kwanza mtu akiniita pasta Christina Shusho, sipo sawa na hilo,” Shusho alifunguka.

Mwezi mmoja baada ya kauli hiyo, John Shusho ambaye ni mhubiri, katoa kauli iliyotafsiriwa sawa na kurusha jiwe gizani, akionekana kumlenga mkewe huyo ambaye pamoja walijaliwa watoto watatu ndoa yao ilipokuwa imesimama.

“Mwambie jirani yako inaumiza, lakini yeye Mungu amesema. Mungu anapotaka kukuandaa kwa jambo fulani, kuna hali fulani ya Kiungu ambayo lazima upite. Hakuna kesho bila maandalizi ya leo. Ili uweze kufika kwenye levo fulani lazima kuwa na maandalizi fulani. Na maandalizi hayo yanaweza yasiwe kwenye matarajio yako. Na kwa sababu hayako kwenye matarajio yako na ni vitu vipya ambavyo vinakutokea, lazima kuna kipindi utaona unapitia kwenye maumivu, lakini Bwana ana mpango na maumivu hayo. Levo mpya, changamoto mpya, ushindi mpya,” Bw Shusho alifunguka wakati akihubiri katika kanisa la Restoration of Hearts hivi majuzi.

Kauli hiyo imetafsiriwa na wengi kuwa ya kumlenga mkewe huyo ambaye kafanikiwa kujijengea himaya ya mashabiki nchini Kenya kutokana na ubinifu wa nyimbo zake kupitia maandiko ya Biblia.

Kwenye ufafanuzi wa kwa nini aliamua kuikimbia ndoa yake, Bi Shusho aidha alisema kuvunjika kwa ndoa yake wala hakukuwa na utata wowote kati yake na mumewe John.

Hata hivyo, kwa mujibu wa John, uamuzi wa Shusho kutoka kwenye ndoa ulimuumiza sana ila ni maumivu anayoamini yalipangwa kwa ajili ya kumuandaa kwa ajili ya msimu mpya katika maisha yake.

Wakati akifungua roho, Bi Shusho alisisitiza kuwa suala la ndoa ni jukumu tofauti kabisa na wito wa Mungu alioupata na hivyo uamuzi wake wa kuondoka katika ndoa yake, ulikuwa sahihi ili kwenda kutimiza mwito wa Mungu.

“Kuoelewa ni sehemu tu lakini alichokiweka Mungu ndani yenu ni vitu viwili tofauti. Mungu anaweza akakuwekea hiki na mimi hiki. Kinachotakiwa tu mfike kwenye makubaliano. Nielewe alicho nacho mwenzangu na yeye aelewe nilicho nacho halafu tuone ni wapi tunaweza kukutania,” alisema Shusho kwenye mazungumzo na bloga mmoja Tanzania.