Michezo

Munala aelezea matumaini tele KCB iko imara

February 11th, 2020 2 min read

JEFF KINYANJUI na GEOFFREY ANENE

KOCHA Japheth Munala anaamini sajili wapya Mercy Moim, Edith Wisa na Sharon Chepchumba wamefanya timu ya KCB kuwa imara zaidi inapotafuta kumaliza ukame wa zaidi ya miaka 30 bila taji la Ligi Kuu.

Klabu hii ilinyakua nyota Moim na Wisa kutoka Kenya Prisons na Chepchumba kutoka Kenya Pipeline mwezi Januari.

Nafasi ambayo KCB imekaribia kutwaa ligi tangu ianzishwe mwaka 1984 ni nambari mbili.

Vipusa wa Munala wameratibiwa kuanza kampeni dhidi ya timu ya kaunti ya Bungoma mapema Ijumaa kabla ya kufufua uhasama na Pipeline adhuhuri siku hiyo mjini Nyeri.

Akizungumza wakati wa mazoezi katika uwanja wao wa Ruaraka, Munala alisema KCB imeiva tayari kukabiliana na yeyote, ingawa akafichua kuwa lengo kubwa ni kuunda kikosi ambacho pia kitatikisa katika Klabu Bingwa Afrika nchini Misri mwezi Aprili.

“Tumekuwa na wachezaji wetu wote mazoezini kwa kipindi cha majuma mawili na nimefurahishwa sana jinsi wamekuwa wakiimarika. Wachezaji wapya wana ujuzi mkubwa na talanta ya hali ya juu. Wanafanya timu hii iwe bora zaidi. Tunajua tuko na wachezaji wazuri wanaoweza kutoka kwenye benchi na kusaidia timu na hicho ni kitu muhimu katika voliboli,” Munala alisema.

“Habari nzuri pia ni kuwa hatuna jeraha lolote na maombi yangu ni kuwa wachezaji wote watasalia katika hali nzuri kimwili na kiafya msimu wote,” alisema na kufichua kuwa baada ya ziara ya Nyeri timu hiyo itazamia shughuli ya kujiandaa kwa Klabu Bingwa.

Aliongeza, “Unaposaini wachezaji wapya, changamoto kubwa huwa ni kupata mshikamano mzuri. Tunahitaji angaa mwezi mmoja zaidi wa kufanya mazoezi pamoja ili tupate mshikamano unaohitajika.”

Licha ya kuongezea kikosi chake nguvu kwa kuvua mastaa hao na kufifisha wapinzani wao, Munala hajatia KCB katika orodha ya mabingwa watarajiwa wa msimu huu.

“Kitu muhimu ni kuhakikisha tunasalia kuwa kitu kimoja na kucheza voliboli ilio na mpango. Voliboli haichezwi na mchezaji mmoja kwa hivyo kila mtu lazima awe katika hali nzuri ndiposa mafanikio yaweze kupatikana. Timu ambayo inafaulu kuwa kitu kimoja kila mara huwa na nafasi nzuri ya kufanya vyema,” alisema.

Munala alijiunga na KCB mwezi Desemba 2018 kutoka Pipeline wakati timu hiyo pia ilisaini wachezaji nyota kutoka Pipeline wakiwemo Leonida Kasaya, Noel Murambi na Violet Makuto.

Kocha huyo anaamini kuwa Pipeline, Prisons Al Ahly kutoka Misri na Watunisia Sfaxien na Carthage wataleta ushindani mkali katika Klabu Bingwa.

Moim, ambaye amechezea klabu nje ya Afrika, anasema ana hamu kubwa ya kuanza maisha mapya KCB kwa kishindo baada ya kuwa na Prisons miaka 13.

“Niko na kumbukumbu nzuri Prisons, lakini sasa mimi ni wa KCB. Nitajitahidi kuisaidia ifanye vyema,” alisema Moim aliyetua Prisons akitokea KCB mwaka 2007 kabla ya kurejea ‘nyumbani’ mwezi uliopita.

Ratiba (Februari 14): Bungoma County na KCB (9.00am), DCI na KDF (9.00am), Kenya Pipeline na Ashton (9.00am), Prisons na Ashton (11.00am), KDF na Bungoma County (11.00am), KCB na Kenya Pipeline (1.00pm).