Mung’aro aacha kanisa gizani kuhusu hospitali

Mung’aro aacha kanisa gizani kuhusu hospitali

NA MWANDISHI WETU

HALI ya suitafahamu imeibuka kuhusu hatima ya hospitali kubwa ya kimishenari ya St Luke’s iliyo Kaloleni, Kaunti ya Kilifi, baada ya serikali ya kaunti hiyo kutangaza mpango wa kujenga hospitali mpya eneobunge hilo.

Awali, serikali ya kaunti iliyoongozwa na aliyekuwa gavana, Bw Amason Kingi, ilikuwa imeweka makubaliano na wasimamizi wa hospitali hiyo iliyofifia kuhusu ushirikiano ambao ungeboresha utoaji huduma kwa umma.

Hata hivyo, Gavana Gideon Mung’aro, sasa ametangaza mpango wa kaunti kujenga hospitali mpya Kaloleni. Hali hii imewaacha wasimamizi wa St Luke’s iliyo chini ya Kanisa la Kianglikana (ACK) kwenye mataa.

Uongozi wa Bw Kingi uliweka makubaliano kushirikiana na hospitali hiyo iliposambaratika hadi kufungwa mwaka wa 2016 ilhali ilikuwa ikitegemewa sana na wakazi wa Kaloleni kwa huduma bora za afya.

Akizungumza katika Wadi ya Mwanamwinga, Bw Mung’aro alisema hospitali mpya itajengwa katikati mwa eneobunge hilo kwa manufaa ya wakazi kutoka pande zote.

“Tutajenga hospitali ambayo itakuwa na vitanda visivyopungua 100 itakayotoa huduma bora za afya kama vile St Luke’s ilikuwa kitambo,” akasema.

Bw Mung’aro aliwataka jamii kutambua sehemu bora ya kujenga hospitali hiyo.

Mbali na hayo, alisema serikali ya kaunti kwa ushirikiano na Chuo Kikuu cha Pwani itajenga hospitali mpya ya mafunzo na rufaa kwenye ardhi ya ekari 89 iliyotolewa na chuo hicho.

Kanisa la ACK likiongozwa na Kasisi Alphonse Baya, lilikuwa na majadiliano na serikali ya kaunti ya awali ya Bw Kingi kuweka mikakati ya kufufua hospitali hiyo na kuimarisha utendakazi kupitia kwa ushirikiano wa kudumu.

Akizungumza na Taifa Leo kwa njia ya simu, Dkt Baya alisema hakufahamu mipango ya serikali ya kaunti kujenga hospitali mpya.

Hata hivyo, alisema hana pingamizi kuhusu mpango huo kwani hakuna ushindani wowote na serikali ya kaunti.

Dkt Baya alisema anatumai kukutana na Bw Mung’aro kwani kanisa la ACK iliweka mkataba na serikali ya kaunti kuhusu hospitali ya St Luke’s.

“Tulikuwa na mkataba na serikali ya kaunti, lakini sasa kuna uongozi mpya. Sikuwa nimekutana na Gavana Mungaro kwa sababu nilikuwa nampa nafasi atulie ofisini. Lakini tukikutana tutaongea kwa kina iwapo watendeleza mkataba huo au la,” akasema.

Kulingana na mkataba huo, serikali ya kaunti ilichukua jukumu la kuajiri wauguzi na madaktari katika hospitali hiyo na pia kupeleka dawa na vifaa vingine vya afya.

Imebainika serikali ya kaunti iliyoondoka ilitoa pia Sh10 milioni kwa ukarabati wa hospitali hiyo.

Dkt Baya alisema bado kuna changamoto kurudisha hospitali hiyo kwa hadhi yake ya zamani kwani inahitaji takriban Sh40 milioni kukarabati na kurejelea huduma zake kikamilifu.

Hospitali hiyo ilianzishwa na shirika la Church Missionary Society (CMS) kutoka Uingereza katika mwaka wa 1927. Ilikuwa chini ya wamishenari hadi mwaka wa 1983 ilipochukuliwa na Kanisa la ACK.

Kusambaratika kwa hospitali hiyo kuliwaathiri zaidi ya wakazi 300,000 kutoka Kaloleni, Ganze, Kauma na Chonyi, ambao walilazimishwa kutafuta huduma katika hospitali ya Mariakani na hospitali ya kaunti ya rufaa ya Kilifi zaidi ya kilomita 20.

Hapo awali, mbunge wa Kaloleni, Bw Paul Katana, alipendekeza hospitali mpya ijengwe akisema hakuna haja serikali ya kaunti iendeleze ushirikiano wake na kanisa la ACK iwapo walidinda kuachia kaunti hospitali hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua aendeleza kauli za kukanganya

TAHARIRI: Miradi ya nyumba za bei nafuu ikamilishwe

T L