Mung’aro alitiliwa sumu, wandani wadai

Mung’aro alitiliwa sumu, wandani wadai

Na Maureen Ongala

WANDANI wa Waziri Msaidizi wa Ugatuzi, Bw Gideon Mung’aro, wamemshauri kujihadhari anapokula katika sehemu za hadhara, baada ya kuzirai alipokuwa akisambaza chakula cha msaada katika Kaunti Ndogo ya Kaloleni wiki iliyopita.

Bw Mung’aro, ambaye tayari asharuhusiwa kurudi nyumbani baada ya kulazwa hospitalini na kutibiwa, alianza kuugua alipokuwa katika ziara Kilifi pamoja na Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo na viongozi wengine wa kisiasa.

Wandani wake wanahofia kuwa, huenda alitiliwa sumu kwa chakula chake katika mojawapo ya hafla alizohudhuria awali.

“Wakati huu wa kampeni za kisiasa, ni lazima Bw Mung’aro ajihadhari. Huenda akawindwa na mahasimu wake wa kisiasa wanaoweza kumtilia sumu,” akadai mmoja wa wandani wake, aliyeomba kutotajwa jina gazetini.

Hata hivyo, Taifa Leo haikufanikiwa kubainisha kwa njia huru chanzo cha ugonjwa uliompata ghafla waziri huyo msaidizi.

Waliohudhuria shughuli za usambazaji wa chakula cha msaada Kadzonzo walisema alianza kuishiwa nguvu akashindwa kuhutubia umma, ndipo akakimbizwa hospitalini.

Mbunge wa Kilifi Kaskazini, Bw Owen Baya, alithibitisha kuwa Bw Mung’aro asharudi nyumbani ila hakutaka kuzungumzia ugonjwa wake.

“Nimezungumza naye, anaendelea vyema. Alitoka hospitalini Mombasa na sasa anapumzika nyumbani kwake Nairobi,” mbunge huyo akasema.

Bw Mung’aro ni mmoja wa wanasiasa wanaolenga kuwania ugavana wa Kilifi mwaka ujao, kuchukua mahali pa Gavana Amason Kingi atakayekamilisha kipindi cha pili cha kuongoza kaunti hiyo.

Hii itakuwa mara yake ya pili kuwania ugavana, baada ya kushindwa mwaka wa 2017 alipowania kupitia kwa Chama cha Jubilee.

Inaaminika amepanga kutafuta tikiti ya Chama cha ODM kuwania wadhifa huo 2022 kutokana na jinsi anavyokaribiana na wanasiasa wa chama hicho katika miezi ya hivi majuzi akiwemo Kiongozi wa chama, Bw Raila Odinga.

Hata hivyo, waziri huyo hajatangaza wazi chama atakachotumia.

You can share this post!

WANTO WARUI: Serikali isaidie kutafuta suluhu kwa visa vya...

Real Sociedad watua kileleni mwa jedwali la Liga baada ya...

T L