Mung’aro ataja baraza lake la mawaziri

Mung’aro ataja baraza lake la mawaziri

NA ALEX KALAMA

GAVANA wa kaunti ya Kilifi Gideon Mung’aro ametaja baraza lake la mawaziri 10 ili kumsaidia kutekeleza manifesto yake katika kipindi cha miaka mitano.

Mung’aro pia amezindua vikosi vitatu vya majopokazi ili kuangalia sekta ya afya, rasilimali, madeni, uchumi na anasubiri kupata ripoti ndani ya miezi miwili.

Akizungumza na waandishi wa wabari nje ya ofisi yake gavana huyo ambaye aliambatana na Naibu wake Florence Chibule pamoja na wawakilishi wadi wengi wa bunge la kaunti hiyo alitaja timu yenye sura mpya kwani alitimua wote waliokuwa katika uongozi uliopita.

Pia aliongeza majukumu mengine muhimu zaidi kwa naibu wake ambayo yatafanywa kupitia amri ya mtendaji kutokana na ratiba yao yenye shughuli nyingi.

“Majukumu yake yatakuwa wazi na kwa mujibu wa katiba na ni pamoja na naibu gavana na taasisi ya gavana kuratibu ushirikiano wa nje, uhusiano na ushirikiano wa kuafikia maendeleo,” alisema Bw Mung’aro.

Mung’aro alisema Chibule pia ataratibu utafiti, kuratibu kazi zozote za serikali ya kaunti, kuratibu maendeleo na utekelezaji wa sera ya elimu ya chekechea (ECD) na utekelezaji wake, na kuratibu utekelezaji wa programu za elimu na utoaji misaada.

Gavana huyo alisema naibu wake pia atamwakilisha gavana katika eneo la Pwani kwenye Jumuiya ya Kaunti za Pwani, akisimamia kitengo cha mikakati na utoaji cha gavana kitakachoundwa hivi karibuni, kutayarisha na kutekeleza mikakati inayoendana na maono ya mwaka wa 2030 na majukumu mengine aliyopewa.

Katika baraza la Mawaziri, Mung’aro alimteua Dkt Ruth Dama Masha awe Waziri wa Jinsia na Huduma za Jamii, Catherine Kenga awe Waziri wa Maswala ya Ujenzi wa Miundomsingi ya Umma na Barabara huku katika Idara za Maji na Mazingira akimteua Omar Said Omar.

Katika sekta ya Utalii na Biashara, Mung’aro alimteua John Ngala huku nafasi ya idara ya fedha na mipango ya uchumi ikimwendea Yaye Ahmed.

Wengine ni Frankline Dena – atakayesimamia idara ya Utumishi wa Umma na Majanga, Peter Mwarogo – Afya na Usafi wa mazingira huku kwa idara ya Ardhi na mipango akimteua Jane Mike Kamto.

Katika idara ya Elimu gavana alimteua Clara Chonga, huku Dkt Peterson Mwangoma akiteuliwa kuongoza idara ya Kilimo na Mifugo.

Vile vile Mung’aro alimteua Joshua Mazera kuwa mshauri wake wa masuala ya uchumi na Henry Lunganje kuwa msimamizi wa masuala ya Kisheria katika kaunti.

“Mawaziri wa kaunti watafanya kazi kwa miaka miwili ijayo na baada ya hapo, tutapitia utendakazi wao ili kuona ikiwa watateuliwa tena au kubadilishwa kwa hivyo inategemea jinsi wanavyofanya bidii kuwahudumia watu wa Kilifi,” alisema Bw Mung’aro.

Kiongozi huyo alisema majina ya wajumbe wake wa baraza la mawaziri yatawasilishwa katika bunge la kaunti ili shughuli ya kuhakiki ianzishwe.

“Tunatumai wataharakisha programu ili tuanze kufanya kazi,” alisema Bw Mung’aro.

Kuhusu majopokazi, alisema lengo ni kumsaidia katika masuala ya utawala na utoaji huduma.

Aidha pi aliagiza afisi ya katibu wa kaunti na idara husika kutoa uwezeshaji na usaidizi unaohitajika ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yake kwa ufanisi na kwa wakati.

Kuhusu jopokazi la utoaji wa huduma za afya, alisema kikosi hicho kitabainisha muundo unaofaa zaidi wa uongozi na utawala unaofaa kwa hospitali ya rufaa ya kaunti na vituo vingine vya afya vya kaunti.

“Chunguza njia za utoaji wa huduma za afya katika hospitali ya rufaa ya kaunti na vituo vingine vya afya vya kaunti. Kutambua njia za kuboresha miundo mbinu ya afya na vifaa ili kuendana na hadhi ya hospitali ya rufaa ya kaunti, na kushughulikia maswala ya rasilimali za watu kama vile mahitaji ya mafunzo ya maendeleo ya wafanyakazi na mambo mengine yote ya kuwajengea uwezo,” alisema Bw Mung’aro.

Vile vile alisema kikosi cha afya pia kitabainisha njia za kuboresha na kufaidika kutokana na ushirikiano na taasisi za mafunzo ya matibabu na vyuo vikuu na pia kuimarisha utafiti.

Mung’aro alisema kikosi hicho kitaundwa na Profesa Rafiq Parker, Christopher Dennis Willson, Benjamin Tsofa, Tabu Ngala, Lorine Omondi, Dkt Masha Mvera, Dkt Abidan Mwachi, Kapteni Dkt Isaac Makorani, na Dkt Osman Abdulahi.

Jopokazi hilo ni la kuangalia muundo wa wafanyakazi na utendakazi wa serikali ya kaunti ya Kilifi ili kubaini muundo wa sasa na kulinganisha na nguvu kazi iliyopo.

Wajumbe wa kikosi hicho alisema ni Fadhil Athman, Jonathan Mativo, Martin Mwaro, Jackson Karisa, Terry Maitha, Damaris Malombe, Flora Kidere, Charles Shia na John Kenga Nyale.

Mbali na hayo Mungaro pia alitaja jopokazi la kuchunguza uhakiki wa bili zinazosubiriwa kuwa ni pamoja na Alice Kinyua, Zaitun Mohamed, Albert Muturi, Dickson Gitonga, Daniel William, Veronica Wanjira , Emily Mulewa, Mwingi Ali na Hazel Katana ambaye alikuwa naibu gavana wa kwanza wa kaunti ya Mombasa katika kipindi cha kwanza cha utawala wa aliyekuwa gavana wa kaunti hiyo Ali Hassan Joho.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool na Spurs kujinyanyua UEFA

Ruto apunguzia Jumwa madaraka

T L