Mung’aro sasa afichua ushirikiano na Jumwa

Mung’aro sasa afichua ushirikiano na Jumwa

NA ALEX KALAMA

GAVANA wa Kilifi, Bw Gideon Mung’aro, amefichua kuhusu ushirikiano uliokuwepo kati yake na Waziri wa Utumishi wa Umma, Jinsia na Haki za Waliotengwa, Bi Aisha Jumwa, kuelekea kwa uchaguzi uliofanyika Agosti 2022.

Akihutubia umma akiwa Ganda, eneobunge la Malindi, Bw Mung’aro ambaye ni mwanachama wa ODM, alisema yeye na Bi Jumwa aliyewania ugavana Kilifi kwa tikiti ya UDA, walikubaliana kuhakikisha mmoja wao ndiye atashinda kiti hicho.

Kulingana naye, makubaliano yao yalikuwa kwamba yeyote atakayeshinda kiti hicho angemuunga mkono yule aliyeshinda wakati akiwa mamlakani kwa kila njia awezayo.

Bw Mung’aro alieleza kuwa, ushirikiano huo wao ulizaa matunda maradufu kwani ni kupitia ushindi wake ambapo Bi Jumwa sasa amefanikiwa kuwa waziri katika serikali inayoongozwa na Rais William Ruto.

“Nilimwambia Ruto juzi kwamba kama singepingana na Aisha kwenye kampeni, kusingekuwa na waziri mwanamke kutoka Pwani,” akasema Bw Mung’aro.

Alikuwa amehudhuria hafla ya maombi na kutoa shukrani ya Bi Jumwa kwa kuajiriwa kuwa waziri.

Katika hafla hiyo, Bi Jumwa alitangaza vita dhidi ya wahalifu wa unyanyasaji wa kiijinsia na wale wanaohusika na mauaji ya wazee katika Kaunti ya Kilifi.

Kwa mujibu wa waziri huyo, mimba za wasichana wa shule, ndoa za kulazimishwa na mauaji ya wazee kwa kisingizio kuwa ni wachawi ni visa ambavyo vimekithiri Kilifi na ni sharti visa hivyo vizimwe.

Alidai kuwa, katika siku za hivi majuzi, baadhi ya wanyanyasaji watoto wamekuwa wakitumia baa la njaa kuwahadaa watoto na kuwadhulumu kingono.

Alitaka Machifu, Polisi, na Kamishna wa Kaunti kuwasaidia waathiriwa wa dhuluma hizo.

“Chifu yeyote atakayebadilisha ubikra wa mtoto wa kike na kuku au mbuzi, nitahakikisha anachukuliwa hatua. Utakula mbuzi na sisi tutakushughulikia,” akasema Bi Jumwa.

Aliwaondolea hofu waathiriwa na kuwataka wajitokeze ili kesi zao ziendelee, na watendewe haki.

“Mimi ni mwathiriwa na ninajua jinsi suala hili lilivyo chungu na linavyoweza kuathiri watu wetu,” akasema.

Waziri huyo alisema ataitisha mkutano na vitengo vya usalama na gavana ili kukomesha dhuluma za kijinsia huko Kilifi na Kenya kwa jumla.

Zaidi ya hayo, alisema wazee wengi wanakufa kwa sababu ya madai ya uongo ya uchawi.

Vilevile, Bi Jumwa alisema kwa kawaida vijana huwaua wazazi wao ili kurithi mali na kuwaonya wahusika kuwa muda si mrefu watafikishwa mahakamani.

“Ningependa kuwaonya wale wanaoua wazee kwa madai kuwa ni wachawi,” alisema.

You can share this post!

Kura ‘ziliuzwa’ kwa Sh600, shahidi adai

Galana-Kulalu kukabidhiwa wawekezaji wa kibinafsi

T L