Habari Mseto

Mungiki, Usiku Sacco na Gaza wahangaisha wafanyabiashara

May 2nd, 2019 1 min read

NICHOLAS KOMU na NDUNGU GACHANE

VISA vya uvamizi unaotekelezwa na magenge ya wahalifu vinazidi kuongezeka katika eneo la Kati huku wataalamu wakilaumu ukosefu wa ajira.

Katika Kaunti ya Murang’a, magenge haramu kama vile Mungiki, Usiku Sacco na Gaza yanayojumuisha vijana wa umri mdogo, yamekuwa yakihangaisha wakazi katika soko za Kandara, Maragua na Mukuyu.

Wakazi wa maeneo hayo waliohojiwa na Taifa Leo, walisema kuwa kundi la Mungiki limefufuka na limekita mizizi katika eneo la Kabati, kaunti ndogo ya Kandara.

Wafanyabiashara na wawekezaji wengineo katika soko hizo sasa wanalazimika kufunga biashara zao saa 12 jioni ili kuepuka kuvamiwa na magenge hayo.

Mwaka 2018, kundi la watu wanane waliodaiwa kuwa wafuasi wa kundi la Mungiki walikamatwa na kushtakiwa katika mahakama ya Kandara kwa kuwa wafuasi wa kundi haramu.

Washukiwa hao walikamatwa katika eneo la Tosheka wakiapishwa kujiunga na kundi la Mungiki, kulingana na upande wa mashtaka.