Mungu ni mkuu, asema mkurugenzi baada ya kuondolewa mashtaka ya wizi wa watoto

Mungu ni mkuu, asema mkurugenzi baada ya kuondolewa mashtaka ya wizi wa watoto

Na RICHARD MUNGUTI

NAIBU wa Mkurugenzi wa huduma za afya katika shirika la utoaji huduma kaunti ya Nairobi (NMS) Dkt Musa Mohammed Ramadhan Jumatatu alimshukuru Mungu nje ya mahakama kuu ya Nairobi baada ya kuondolewa mashtaka ya wizi wa watoto katika hospitali ya Mama Lucy Kibaki mwaka uliopita.

“Namshukuru Mungu kwa kuniondolea kesi niliyoshtakiwa nayo mwaka jana. Kama vile nilivyosema mbeleni kwamba sikuhusika na wizi wa watoto, hivyo ndivyo polisi wamepata baada ya uchunguzi wa kina. Sasa niko huru,” alisema Dkt Ramadhan alipohojiwa na Taifa Leo baada ya kuachiliwa.

Mshtakiwa huyo alipiga magoti nje ya mahakama kuu ya Milimani na kusema “(Alahu Akbara) Mungu ni mkuu”. Watu wa familia yake waliofika mahakamani kufuata kesi walifurahi wote.

Wote nje ya mahakama wakiongozwa na Dkt Ahmed Kalebi walisema “Alahu Akbar”. Dkt Ramadhan alipiga bismilahi tatu kisha akaanza kudodokwa na machozi.

Watu wa familia yake waliandamana kuenda nyumbani. “Tutasherehekea nyumbani,” Dkt Kalebi aliambia Taifa Leo.

Naibu wa Mkurugenzi wa huduma za matibabu kaunti ya Nairobi Dkt Musa Ramadhan asujudu nje ya mahakama ya milimani baada ya kuondolewa mashtaka ya kuwaiba watoto alipokuwa kinara wa hospitali ya mama Lucy na kuwauza. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Alisema Dkt Ramadhan amekuwa kielelezo chema kwa watu wa jamii ya Wanubi nchini “ikitiliwa maanani tuko na madaktari watano tu.”

Dkt Ramadhan alisema amewasamehe waliomwekelea madai ya uwongo.

“Sitaishtaki Serikali kwa kuniharibia sifa haswa kuniusisha na wizi wa watoto wachanga. Vile nimeondolewa lawama sina chuki na yeyote na nitaendelea kutoa huduma zangu kama hapo mbeleni,”alisema Dkt Ramadhan.

Daktari huyo aliondolewa lawama miezi minne baada ya madaktari wakuu katika hospitali hiyo Dkt Emma Mutioa na Dkt Regina Musembi kuachiliwa.

Madaktari hao wakuu walitiwa nguvuni kufuatia ufichuzi katika shirika la habari la BBC kwamba kuna kashfa inayoendelea na kuwauza watoto.

Shirika hilo lilitangaza kuwa watoto walikuwa wakiibwa kutoka kwa kina mama maskini na kuuzwa na maafisa wa hospitali hiyo kwa bei ya Sh45,000.

Dr Ramadhan aliondolewa mashtaka baada ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) kusema hakua ushahidi wa kumuhusisha na kashfa hiyo.

Watu wa familia yake waliofika mahakamani kufuata kesi walimpa busu. PICHA/ RICHARD MUNGUTI

Akiwasilisha ombi la kutamatisha kesi dhidi ya Dkt Ramadhan kiongozi wa mashtaka Bi Evalyene Onunga alimweleza hakimu mwandamizi Bi Esther Kimilu kuwa sasa mshtakiwa huyo(Ramadhan) atakuwa shahidi katika kesi dhidi ya maafisa wa masuala ya kijamii hospitalini humo Bw Makallaa Fred Leparan na Selina Adundo Awuor.

Bi Kimilu alitamatisha kesi dhidi ya Dkt Ramadhan kisha “akaamuru mshtakiwa arudishiwe dhamana ya Sh200,000 pesa tasilimu aliyokuwa amelipa kortini.”

Punde tu baada ya kuachiliwa kwa kinara huyo wa huduma za matibabu kaunti ya Nairobi shahidi wa kwanza, wakili Brian Kimeu Muia alisimulia jinsi alimuokota mtoto mchanga aliyekuwa ametupwa ndani ya kibanda cha kuuzia mboga kwenye barabara ya Outering Nairobi.

Bw Muia aliyekuwa na rafikie Bw Morris Nguyo Muki walimsikia mtoto huyo mchanga akilia kwa kutoa sauti kama ya Paka.

“Morrris alinieleza sauti hiyo ni ya jini..Nilimueleza hata mimi sijawahi ona jinni tuingie kibandani tumwone,” Bw Muia alisimulia.

Shahidi huyo alisema walimpeleka mtoto huyo kwa mzee wa kijiji mtaani Savana na hatimaye wakampeleka kituo cha polisi.

“Nilipewa barua nimpeleke hospitali ya mama Lucy ambapo tulimkabidhi Bw Leparan.

“Mtoto huyo aliyekuwa mchanga alipelekwa kuhifadhiwa katika idara ya watoto kisha nikamwandikia barua Dkt Ramadhan nikiomba niruhusiwe kumridhi mtoto huyo niliyempa jina Taji,” Bw Muia alisema.

Bw Muli aliyetoa ushahidi pia alitahadharishwa dhidi ya kuongea lugha ya Sheng kortini.

“Hiyo lugha unayoongea hapa kortini ya Sheng sio rasmi. Zugumza kishwahili sanifu,” Bi Onunga alimweleza Bw Muli.

Bw Muli alikuwa ameeleza mahakama jinsi yeye na Bw Muia na marafiki wengine walienda “kupiga tembo (kubugia pombe) kuchangamkia ubabe wa rafiki yao katika biashara yake.”

Aliposema hayo Bi Kimilu alimwuliza shahidi alichokuwa akisema na kuonywa asizugumze lugha ya sheng kortini.

Bw Muli alianza kuzugumza Kiswahili sanifu na kusimulia jinsi walimuokota mvulana aliyekuwa amezaliwa Mei 4 2020 na kutupwa.

Kesi inaendelea.

You can share this post!

Askofu aonya wanaume dhidi ya kutumia ‘viagra’...

Joho alipa Sh1m kuwania tiketi ya urais ya ODM kabla ya...