Munya ahimiza wakulima wakumbatie teknolojia za kisasa

Munya ahimiza wakulima wakumbatie teknolojia za kisasa

NA SAMMY WAWERU

UKUAJI katika sekta ya kilimo utaafikika kikamilifu kupitia mifumo ya teknolojia za kisasa.

Waziri wa Kilimo, Peter Munya amesema uhaba na usalama wa chakula nchini utaangaziwa wakulima wakikumbatia vumbuzi na teknolojia kuendeleza zaraa.

Huku athari za tabianchi zikiendelea kuhangaisha mazingira na shughuli za kilimo, Bw Munya amesema malengo ya kitaifa kukabili baa la njaa yatafanikishwa kupitia mifumo ya kisasa kuboresha kilimo.

Munya alisema hayo kupitia ujumbe uliosomwa na Waziri Msaidizi katika Wizara, CAS Lawrence Omuhaka, wakati wa ufunguzi rasmi wa Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa 2022, katika ukumbi wa KICC jijini Nairobi.

Waziri Msaidizi katika Wizara ya Kilimo, CAS Lawrence Omuhaka, akihutubu katika hafla ya ufunguzi rasmi Makala ya Saba Maonyesho ya Kimataifa Agritech Africa, KICC Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

Maonyesho hayo ya Makala ya saba, yalihudhuriwa na kampuni, mashirika na taasisi kutoka ndani na nje ya nchi, yaliyotumia jukwaa hilo kuonyesha teknolojia za kisasa kuboresha kilimo na ufugaji.

Mashine na mitambo ya kileo, pia ilionyeshwa, wakulima na wafugaji wakikongamana kutoka maeneo tofauti nchini.

“Mbali na kuongeza mazao, mifumo ya kisasa inayaboresha kuwa ya hadhi kuteka masoko yenye ushindani mkuu,” taarifa ya Bw Munya ikaelezea.

Baadhi ya waonyeshaji walitoka mataifa kama Ujerumani, China, Uturuki, India, Marekani, Pakistani, Sri Lanka na Brazil, nchi ambazo zimebobea kiteknolojia kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji.

Kando na mashine na mitambo, vifaa vya maandalizi ya shamba, upanzi, kupalilia, uvunaji maji na unyunyiziaji pia vilionyeshwa.

Waliojitokeza vilevile walipata mafunzo ya kilimo endelevu na bora, mavuno, mbinu za kukabiliana na majanga, ikiwa ni pamoja na mifumo ya uongezaji thamani.

Isitoshe, teknolojia katika ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kuku zilivutia wafugaji, kuanzia uzalishaji hadi uongezaji mazao thamani ili kukwepa kero ya mabroka.

“Mashirika na kampuni, yanayojihusisha na teknolojia za kilimo yajitokeze tuboreshe sekta hii ambayo huchangia asilimia 33 katika ukuaji wa uchumi, GDP,” waziri Munya akahimiza.

Mada ya maonyesho hayo ilikuwa ‘Uboreshaji Mapato ya Wakulima Kupitia Uvumbuzi na Teknolojia’, Wizara ya Kilimo ikisisitiza inaambatana na baadhi ya Ajenda Nne Kuu za Serikali; Usalama wa Chakula na Viwanda.

Serikali kupitia sekta ya viwanda – uongezaji thamani mazao ya kilimo inalenga kuingiza kima cha Sh23.4 bilioni kwa mwaka na katika malengo 17 ya SDGs yaliyopitishwa na marais na viongozi kutoka nchi mbalimbali ulimwenguni 2015.

“Hivyo basi, tunahimiza wakulima na washirika katika mtandao wa uzalishaji chakula nchini kukumbatia mifumo ya teknolojia ya kisasa tuafikie asilimia 100 ya usalama wa chakula,” Bw Omuhaka akasema, akiahidi kwamba serikali imejitolea mhanga kuimarisha sekta ya kilimo.

Maonyesho hayo yaliandaliwa na Radeecal Communications, Afisa Mkuu Mtendaji, Sanyal Desai akidokeza kuwa kampuni na mashirika 156 hususan yenye mchango kupitia mifumo na teknolojia za zaraa yalishiriki.

Waziri Msaidizi Wizara ya Kilimo, CAS Lawrence Omuhaka, Afisa Mkuu Mtendaji Radeecal Communications, Bw Sanyal Desai (aliyevalia koti la kijani), wakionjeshwa bidhaa zilizoongezwa thamani wakati wa ufunguzi rasmi Makala ya Saba Maonyesho ya Kimataifa Agritech Africa, KICC Nairobi. PICHA | SAMMY WAWERU

“Usalama wa chakula duniani kwa sasa ndio hoja kuu, wadau na wahusika watumie majukwaa kama haya kuungana kupiga jeki sekta ya kilimo,” Bw Sanyal akasema.

Maonyesho hayo ya siku tatu, yalirejea miaka mitatu baada ya kusitishwa kwa muda kufuatia mkurupuko wa janga la Covid-19 nchini, 2020.

“Kenya inahitaji mifumo ya teknolojia za kisasa kuboresha shughuli za kilimo. Ipo ya wakulima wa mashamba madogo na yale ya kadri, ambayo bila mvua uzalishaji chakula utaendelea,” Sanyal akaelezea.

Afisa huyo aidha aliishukuru serikali ya Kenya, kupitia mchango wake kufanikisha maonyesho hayo.

Aidha, Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa, yalizinduliwa nchini 2014.

  • Tags

You can share this post!

VALENTINE OBARA: MCAs waelezee wanayokamia kufanyia raia...

Daraja la juu ya Thika Superhighway kujengwa Juja

T L