Habari MsetoSiasa

Munya ataka thamani ya pamba iimarishwe

August 19th, 2019 2 min read

Na FADHILI FREDRICK

WAZIRI wa Biashara na Viwanda, Bw Peter Munya ametoa wito kwa wawekezaji kuongeza thamani zaidi kwenye zao la pamba ili kutoa nafasi za ajira nchini.

Alisema ikiwa nchi itaendelea kusafirisha pamba kwa mataifa ya nje ikiwa haijaongezwa thamani basi itaijenga uchumi wa nchi zingine bila kufaidi wakulima wa humu nchini.

Kulingana naye, ni kwa msingi huu ambapo serikali iliamua kuzuia usafirishaji wa pamba nje ya nchi.

“Tumekuwa tukizuia usafirishaji wa pamba kwa sababu tunataka viwanda kama Rivatex na vingine ambavyo tunandelea kivifufua kupata malighafi ya kutosha ili kuendeleza shughuli zao,” akasema Bw Munya.

Aidha alisema hatua hiyo imelenga kuzuia hasara ya kiuchumi itakayotokea ikiwa pamba itasafirishwa bila kuongezwa thamani na kujenga uchumi wa nchi zingine.

Bw Munya alikuwa akizungumza katika ziara ya kukutana na wakulima wa pamba kaunti ya Kwale.

Wakulima hao walikusanyika chini ya muungano wa Ushirika wa Pamba na Viazi (PAVI) ambao ulizinduliwa mnamo 2016 ukiwa ni mpango wa pamoja kati ya kampuni ya madini ya Base Titanium, Cotton On Group (COG) na Business for Development (B4D).

Ushirika huo unajumuisha wakulima wa kipato cha chini katika kaunti hiyo na ina wanachama takribani 3,000.

Vile vile waziri huyo iliwahakikishia wakulima kuwa serikali ina mpango kabambe wa kushughulikia maswala yanayowaathiri.

Aliwahimiza wakulima wadogo wadogo kuungana ili wafaidi huduma za serikali kwa kuwapa rasilimali kuendeleza kilimo cha zao hilo

Kwa upande mwingine Bw Munya aliwataka Wakenya kununua bidhaa zilizotengenezwa nchini, akisema wakenya wanakasumba ya kununu bidhaa za ng’ambo wakisema huwa ni thabiti.

“Wakenya wana tabia ya kutonunua nguo mpya za ndani sio kwa sababu ni ghali lakini kuna shida ya mtazamo na Wakenya wakidhani kwamba bidhaa kutoka nchi zingine ni za hali ya juu,” akasema.

Mwenyekiti wa Pavi Bwa Mahmoud Masemo alitoa changamoto kwa serikali kusaidia wakulim na mbegu za kisasa na mikopo itakayo wawezesha kupata faida kubwa kutoka kilimo cha pamba.