Munyes na Keter waitwa na Seneti kuhusu bei ya mafuta

Munyes na Keter waitwa na Seneti kuhusu bei ya mafuta

Na CHARLES WASONGA

MASENETA wamewaita Waziri wa Petroli John Munyes na mwenzake wa Kawi Charles Keter kufika mbele yake Jumanne wiki ijayo kujibu maswali kuhusu ongezeko la bei ya mafuta.

Spika wa Seneta Kenneth Lusaka Jumatano jioni aliwaamuru mawaziri hawa wawili kufika, binafsi mbele ya kikao cha bunge lote bila kuchelewa.

“Naamuru kwamba kamati ya Kawi iwaite mawaziri wawili wahusika. Waziri wa Kawi na mwenzake wa Petroli pamoja na wakuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Kawi Nchini (Epra) wafike mbele yake Jumanne wiki ijayo kuangazia suala hili lenye umuhimu wa kitaifa. Mkutano huo utafanyike katika ukumbi huu na uhudhuriwa na maseneta wote 67,” akasema.

Alisema hayo kufuatia ombi ambalo liliwasilishwa na Seneta wa Nandi Samson Kiprotich Cherargei aliyetaka ufafanuzi kuhusu ni kwa nini serikali iliongeza bei ya mafuta kupita kiasi na hivyo kuwaathiri wananchi.

Katika ombi lake, Bw Cherargei anataka mawaziri hao wawili kuelezea ni kwa ni serikali ilikatiza nafuu ruzuku kwa bei ya mafuta ya kima cha Sh1.4 bilioni ambayo imekuwepo kuanza Machi mwaka huu. Ruzuku hiyo ilizuia kuongezwa kwa bei ya mafuta kwa kiasi ambacho Wakenya hawangemudu ikizingatiwa kuwa wanaathirika na janga la Covid-19.

“Vile vile, tunataka mawaziri hao waeleze ni kwa nini bei ya mafuta imekuwa ikipanda kwa miezi kadhaa pasina Epra na Wizara uchukua hatua kudhibiti bei hiyo,” akasema Bw Cherargei.

Seneta huyo pia anataka Mbw Munyes na Keter kuelezea hali ya mradi wa uchimbaji mafuta wa Ngamia 1 kaunti ya Turkana, pesa ambazo serikali ilipata kutokana na mauzo ya mafuta hayo na jinsi fedha hizo zilivyotumika.

Isitoshe, Bw Cherargei anataka serikali ieleze ni kwa nini bei ya mafuta ni nafuu katika mataifa jirani ya Uganda, Tanzania na hata Somalia. Hii ni licha ya kwamba kwa mfano, mafuta yanayouzwa Uganda hutua katika bandari ya Mombasa na kusafirishwa kwa barabara na reli hadi nchini humo.

Katika nyongeza iliyotolewa na Epra Jumanne usiku, bei za petrol, dizeli na mafuta taa zilipandwa kwa Sh7.58. Sh7.97 na Sh12.97, mtawalia.

Kutokana na nyongeza hiyo bei ya petrol jijini Nairobi na Sh134.72, dizeli ni Sh115.60 na mafuta ni Sh110.82 kwa lita moja.

Hatua hii itaongeza gharama ya maisha kwa Wakenya kwa ujumla, kupitia nyongeza ya nauli, bei za bidhaa zinazotengezwa viwanda, bei ya stima, na gharama za kilimo kwa kutumia mitambo ya kisiasa inayotumia dizeli.

Sababu kuu inayochangia nyongeza ya bei za mafuta ni kupanda kwa aina mbalimbali za ushuru zinazotozwa bidhaa hiyo.

Kwa mfano ushuru wa ziada ya thamani kwa petrol imepanda hadi kiwango cha asilimia 9.98 kutoka asilimia 8.

Hii imechangia kupanda kwa jumla ya ushuru zinazotozwa petrol kufika Sh58.81 kutoka Sh56.42 kwa lita moja mnamo Machi mwaka huu.

Serikali pia imeongeza aina mbalimbali za ushuru zinazotozwa dizeli, inayotumika katika sekta ya uchukuzi, kilimo na uzalishaji stima, kiasi kwamba wakati huu lita moja ya bidhaa inatozwa Sh46.46 kutoka Sh44.79 mwezi Machi mwaka huu.

Lita moja ya mafuta taa ambayo inatumika kwa wingi na rais wenye mapato ya chini kupitia na kuwasha taa, sasa inatozwa jumla ya Sh41.14 kama ushuru.

You can share this post!

Ruto ainua mikono, asema yuko tayari kuridhiana na Uhuru...

Muturi atoa ishara anaelekea kwa Ruto