Michezo

Muokoko aweka rekodi ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kiumri kuwahi kutandaza soka ya UEFA

December 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

CHIPUKIZI Youssoufa Moukoko aliweka historia ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa katika kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Hii ni baada ya waajiri wake Borussia Dortmund kumpanga kwenye kikosi kilichotandika Zenit St Petersburg 2-1 katika mechi ya Kundi F mnamo Disemba 8, 2020.

Ushindi huo uliwasaidia Dortmund kukamilisha kampeni zao kileleni mwa Kundi F ambalo pia linajumuisha Lazio ya Italia na Club Brugge ya Ubelgiji.

Akiwa na umri wa miaka 16 na siku 18 pekee, Muokoko aliingizwa uwanjani katika kipindi cha pili cha mchuano huo uliosakatiwa nchini Urusi.

Wenyeji walifungua ukurasa wa mabao kupitia Sebastian Driussi katika dakika ya 16 kabla ya Dortmund ya Ujerumani kufingiwa mabao mawili ya haraka na Lukasz Piszczek na Axel Witsel katika dakika za 68 na 78 mtawalia.

Lazio nao walifuzu kwa hatua ya 16-bora wakishikilia nafasi ya pili kundini baada ya kusajili sare ya 2-2 dhidi ya Club Brugge waliokamilisha mechi wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani.

Dortmund ambao pia wanajivunia chipukizi Jude Bellingham, Erling Braut Haaland na Jadon Sancho, huenda sasa wakakutana na FC Porto au Sevilla kwenye hatua ya mwondoano.

Kabla ya Muokoko, wachezaji wengine wachanga zaidi waliowahi kuwajibishwa kwenye UEFA ni aliyekuwa sogora wa Anderlecht ya Ubelgiji, Celestine Babayaro (miaka 16 na siku 87) aliyeonyeshwa kadi nyekundu dhidi Steaua Bucharest mnamo 1994.

Muokoko aliweka rekodi ya kuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga). Droo ya hatua ya 16-bora ya UEFA imeratibiwa kufanyika Disemba 14, 2020.