Habari

Murang'a ndiyo kaunti fisadi zaidi Kenya – Ripoti

March 27th, 2018 2 min read

Na CECIL ODONGO

KAUNTI ya Muranga’a ndiyo fisadi zaidi kati ya kaunti zote 47 humu nchini kulingana na ripoti iliyozinduliwa Jumanne na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) katika jumba la KICC jijini Nairobi.

Kiwango cha hongo katika kaunti hiyo ni asilimia 90.7 ikifuatwa na Trans Nzoia (80%), Mandera (79.4%), Kirinyaga (78.9%), Marsabit (78.2%), Tharaka Nithi (75.7%), Meru (70.8%), Laikipia (69.7%), Machakos (62.7%) na Nyandarua(61.5%) katika orodha ya kaunti kumi ambako ufisadi umekita mizizi.

Kulingana na ripoti hiyo iliyohusisha mahojiano katika nyumba 5,908 kutoka kaunti zote 47, ufisadi katika utoaji zabuni, mfumo wa mapendeleo wa kuajiri na maafisa wa kaunti kutoa huduma kwa kuitisha hongo ni baadhi ya vigezo vilivyotumika

Kwa upande mwingine kaunti za Lamu (5.8%),Taita Taveta (8.3%), Tana River (12.1%), Kericho(12.4%) na Wajir (14.7%) zina viwango vya chini vya ufisadi.

Lengo kuu la utafiti huo ni kutathmini hatua ambazo zimepigwa kupambana na uovu huo na kuweka mikakati mahususi ya kukabiliana nao.

Kati ya wale waliohojiwa, asilimia 80 wana mtazamo kwamba kiwango cha ufisadi kingali juu nao asilimia 40 kati yao wanaamini ufisadi unaongezeka kila kukicha.

 

Polisi wazidi kuongoza kwa ulaji rushwa

Kwenye uorodheshaji wa taasisi za serikali Idara ya Polisi waliibuka kidedea katika upokeaji hongo kwa mwaka wa tisa mfululizo wakifuatwa na wenzao polisi wa trafiki, hospitali za umma, Idara ya Uhamiaji na usajili wa watu kisha Hazina ya ustawi wa Maeneobunge, CDF.

Hata hivyo matumaini makubwa ya wakenya wazalendo wanaokemea ufisadi yako kwa vyombo vya habari kwa asilimia 70.3, vyombo vya habari vya kibinafsi asilimia 69.6, wanadini asilimia 63.8, Mamlaka ya Urais asilimia 49.3 na EACC asilimia 43.9.

Wizara ya Usalama wa Ndani, Afya, Ugatuzi, Uchukuzi na Ardhi pia zinashuhudia wanaotafuta huduma za serikali wakishiriki ufisadi pakubwa.

Wizara ya Maji, Bunge, wizara ya Madini na ofisi ya Mwanasheria Mkuu ziko bora katika kuwapa wananchi huduma bila kutoa ‘kitu kidogo’.

Kiwango jumla cha hongo kinachotolewa na kila mwananchi katika kaunti kiliongezeka kutoka Sh 5,648.50 mwaka wa 2015 hadi Sh7,081.05 mwaka uliopita.

Maafisa kutoka kaunti za Meru, Kajiado, Elgeyo-Marakwet, Kiambu na Baringo ndiyo wanaongoza katika kuitisha hongo kutoka kwa umma.Nazo Kaunti za Busia, Tharaka Nithi, Nairobi, Lamu na Isiolo zikikusanya kati ya Sh80,000 hadi Sh13,000 kabla kutoa huduma muhimu kwa umma.

Akizungimza kwenye uzinduzi huo Mwenyekiti wa tume hiyo Askofu mkuu mstaafu Eliud Wabukala aliwataka wananchi wote kuwa katika mstari wa mbele kuhakisha kwamba jinamizi hilo linatokomezwa akitaja ufanisi uliopigwa na tume hiyo tangu achukue usukani.