Makala

MURANG'A: Wanawake waliolaani wanao hutakaswa kupitia ngono hadharani

May 28th, 2019 4 min read

Na MWANGI MUIRURI

MZEE Muiruri Waithaka (pichani) katika kijiji cha Rwanganga, Kaunti Ndogo ya Kigumo, Kaunti ya Murang’a hujipa riziki ya kando kupitia kutakasa wanawake ambao wamelaani watoto wao kupitia kuvunja vyungu vilivyojaa chakula.

Lakini njia yake ya utakaso imezua mjadala mkuu katika jamii ya Agikuyu kwa kuwa utakaso wake huwa ni kufanya mapenzi hadharani na mwanamke huyo ambaye amelaani.

Wakati kumeripotiwa mwanamke ambaye amelaani watoto wake kupitia hali hiyo, Bw Waithaka husakwa na bila kujali umri wa mwanamke huyo, bila kutumia kinga, bila kujali kama huyo mwanamke ana mume au hana, hufanya mapenzi naye hadharani na tena mchana kukiwa na mashahidi.

Kulingana na mila na desturi za jamii ya Agikuyu, laana hiyo ya kuvunja nyungu ikiwa imejaa chakula huchukuliwa kwa uzito zaidi kwa kuwa mwanamke wa jamii hiyo husemwa ametunukiwa baraka na Maulana ya vyungu viwili maishani mwake, ile ya uzazi na ile ya upishi, ya upishi ikiwa ni ya kulisha vizazi vya ile ya uzazi.

Laana hii ya kuvunja nyungu huchukuliwa kwa uzito zaidi na walengwa wa hasira ya mama huyo, na hiuorodheka pamoja na laana ambapo kwa hasira, mama atalaani kwa kutaja sehemu zake za uzazi, matiti au nywele katika sehemu zake za uke.

Wakati mama amelaani kwa kiwango hicho, taharuki ambayo hutanda ndani ya maisha ya watoto wake huwa ni kuu, na katika kusaka afueni, hakuna kile wanachoweza wakaambiwa watekeleze ambacho bora watamudu gharama, watakosa kukifanya kama njia ya kujitakasa kutokana na laana hiyo.

Ni katika hali hiyo ambapo Bw Waithaka amejipa nafasi ya kuvuna pato ambapo kuna uwiano wa kimaoni katika baadhi ya wazee wa kijamii kuwa njia ya kipekee ya kutakasa laana ya aina hiyo ni kukejeli ile nyungu ya uzazi ambayo inamilikiwa na huyo mama kupitia kuichafua, sawa na vile amechafua mila na desturi kupitia kulaani akitumia nyungu yake ya upishi.

Mbakaji

Shida ni kwamba, baada ya kugunduliwa vile Bw Waithaka amekuwa akitakasa wanawake hao, mjadala mkuu umezuka, wengine wakimpuuza na kumtaja kama ‘gaidi mbakaji wa kijamii’.

Lakini Bw Waithaka mwenye umri wa miaka 59 anajitetea akisema kuwa haoni ni kwa nini ameanza kuvutia hisia hasa za pingamizi, akisema kuwa “mimi huwa tu naalikwa na huwa nalipwa Sh500 za pombe, Sh200 za chakula na baada ya tendo hilo la utakaso, huwa nalipwa Sh2, 000.”

Anasema kuwa alifanya utakaso huo mara ya mwisho Aprili 28, 2019 katika kijiji cha Kandani, na kwamba kuna baraza la wazee wa jamii ya Agikuyu ambalo mwaka wa 1965 lilitoa uamuzi wa jinsi utakaso wa laana hiyo ya mama kuvunja nyungu unatekelezwa.

“Mimi baada ya kuzaliwa mwaka wa 1960 nimekuwa katika jamii ambayo inatekeleza utakaso huo kwa hii njia. Mimi nimerithi tu mila na desturi na ikiwa watangulizi wangu hawakulaaniwa kwa kushirikisha utakaso huu, mbona mimi nianze kuchukuliwa kama anayefanya jambo ambalo ni la kipekee?” akajitetea katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo Dijitali. 

Anasema kuwa “ninyi watu wa vyombo vya habari ndio mnavuruga mambo hapa. Sijui ni nani amewaelekeza kwangu…lakini sina la kuficha. Mimi huwa natakasa wanawake ambao wamelaani familia zao na hata ukipata wateja, nitashukuru ukinielekeza kwao,” asema.

Kwa mujibu wa mtafiti, mwalimu na mshauri kuhusu mila na desturi za Agikuyu, Chifu Kanyonga wa Mukono, utakaso huo wa Bw Waithaka ni kinyume na itikadi za jamii ya Agikuyu.

Kuharibu sifa ya Agikuyu

“Hakuna popote katika mila na desturi za Agikuyu ambapo ngono kati ya watu wawili ilitumika kama utakaso. Hakuna tambiko la aina hiyo katika jamii yetu. Kile hutakasa ni damu ya mnyama hasa mbuzi lakini sio ngono. Kufanya hivi ni kuharibu sifa nzuri za jamii ya Agikuyu,” asema.

Anasema kuwa tambiko lingine huwa ni kutumia matumbo ya mbuzi ambapo aliyelaani hufanywa atapike laana hiyo ametoa…

“Ni laana kufanya mapenzi na mwanamke mchana na hadharani. Huwezi ukasema ukifanya hivyo unatakasa chochote. Huu ni uhaini mkuu wa kitamaduni nan i utapeli mkuu wa kijamii ambapo kunao wanaendesha uongo kuwa hii ni njia ya kutakasa,” asema.

Hayo yakijiri, Bw Waithaka anasema kuwa “sioni ni kwa nini nipingwe kwa kiwango hicho. Mimi huwa sirandarandi nikisaka wa kutakasa. Mimi sichochei wanawake walaani familia zaio ili niitwe nikawatakase…Mimi hujipata tu nimeitiwea kazi na badala ya kunilaumu, nafaa kupewa hongera kwa kuhatarisha maisha yangu ili watoto wengi wa Agikuyu waponyoke laana za mama zao.”

Watetezi wa haki za wanawake eneo hilo la Murang’a wakiongozwa na Cecilia Njogu wanasema kuwa hii ni dhuluma kuu dhidi ya wanawake.

“Huwezi ukamshirikisha mwanamke katika ngono ya hadharani kukiwa na mashahidi na utwambie kuwa unatakasa laana…Huo ni ubakaji, dhuluma kuu dhidi ya wanawake na ambayo tutapinga kwa dhati,” asema.

Kinyume cha sheria

Kamanda wa Polisi wa Murang’a, Josephat Kinyua anataja mila hii ya utakaso kuwa “yuenye shaka kuu kisheria.”

Anasema: “Aaaii! Nipate fununu huyu mwanamume atakuwa wapi tena akitakasa kwa njia hiyo, usiwe na shaka kuwa nitamtia mbaroni ikiwa atakuwa akifanya hiyo kazi mahali mimi nasimamia kiusalama.”

Anasema kuwa hakuna uhalali kisheria kushirikisha mwanamke kufanya tendo la ndoa hadharani.

“Sheria haikubali. Sisi hutekeleza sheria wala sio mila. Ningeomba wazee wa kijamii washikane mkono na watoe mwongozo halali kuhusu utakaso unaohitajika na ambao unatilia maanani haki za kibinadamu na uhalali wa kisheria,” asema.

Bw Joseph Kaguthi ambaye ni mmoja wa wazee wa baraza la jamii hiyo anasema kuwa hakuna mwongozo rasmi wa utakaso kuhusu mwanamke ambaye amelaani kwa kiwango cha kuvumnja nyungu.

“Ndiyo sababu pengo hilo linajazwa na wengine kupitia mikakati kama hiyo ya Bw Waithaka na ambayo kwa uhakika ni haramu. Lakini kwa wale ambao wanaelewa kwa undani kuhusu taharuki ya laana ya kuvunja nyungu, wataelewa kuwa hii ni njia moja tu ya kusaka afueni lakini katika macho ya usasa na sheria, sio mwafaka,” asema.

Anasema kuwa Bw Waithaka alipata tu mwanya wa kuunda pesa na akaukumbatia, akiwa hana nia mbaya, lakini katika mtazamo wa uchambuzi kwa kina, amejipata katika mkondo mbaya.

“Hasa ni hatari ikizingatiwa kuwa huwa hatumii kinga, kuna mashahidi ambao hutazama utakaso huo ukitekelezwa na kuwa huwa sio kwa hiari hivyo basi kuishia kuwa kama dhuluma. Hii ni mojawapo ya mila ambayo imepitwa na wakati,” asema.

Bw Kaguthi anasema kuwa wazee wa kijamii wanafaa kutoa mwongozo wa kufuatwa katika utakaso wa laana.

Lakini aliyekuwa Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki katika Kaunti ya Nyeri, Peter Kairo anasema kuwa “ndio kuna mila na desturi za kijamii lakini pia usisahau kuna aliye mkuu katika maisha hayo yote na ambaye ni Mungu muumba wa ardhi na mbingu.”

Anasema kuwa mila na desturi ambazo hazina uwiano na mapenzi ya Mungu hazifai kutekelezewa yeyote.