HabariSiasa

Murathe afichua kiini cha uhasama wake na Ruto

February 7th, 2019 2 min read

Na WANDERI KAMAU 

ALIYEKUWA Naibu Mwenyekiti wa Chama cha Jubilee (JP) David Murathe ametaja matatizo yaliyotokea kwenye teuzi za chama mnamo 2017 kama sababu kuu za tofauti kati yake na Naibu Rais William Ruto.

Kwenye mahojiano na kituo kimoja cha televisheni Jumanne usiku, Bw Murathe alikubali kwamba uteuzi huo ulikumbwa na hitilafu, hali iliyochangia baadhi ya wanasiasa maarufu kushindwa, hasa katika maeneo ya Mlima Kenya na Bonde la Ufa.

Dkt Ruto ndiye alikuwa msimamizi wa shughuli hizo, ambapo zilipangwa kutoka makao makuu ya chama hicho katika jumba la Jubilee House.

“Tofauti zangu na Ruto zilianza baada ya kuvurugika kwa awamu ya kwanza ya uteuzi wa Jubilee. Kulikuwa na matatizo mengi sana ambayo yalitokea, ila baadhi ya wasimamizi wakuu wa chama hawakuwa na ufahamu wowote. Hilo lilikifanya chama kuandaa shughuli mpya za uteuzi,” akasema.

Bw Murathe alieleza kwamba hali ilizidi kudorora baada ya kuandaliwa upya kwa shughuli hizo, kwani “watu wenye ushawishi waliziingilia ili kuhakikisha kwamba walioshinda ni wale waliowapendelea.”

“Tulibaini kwamba kulikuwa na mipango iliyowekwa kuhakikisha kuwa baadhi ya wanasiana maarufu wamependelewa dhidi ya wengine,” akasema Bw Murathe.

Alitaja hilo kama sababu kuu iliyofanya uhusiano wao na Dkt Ruto kudorora, kwani lengo lake kuu lilikuwa ni kubuni kundi la wanasiasa ambao wangemsaidia kujinadi kisiasa, kwenye azma yake kuwania urais mnamo 2022.

Kiongozi huyo alieleza kwamba walishindwa kushughulikia malalamishi yaliyowasilishwa na wanasiasa hao, kwani lengo lao kuu lilikuwa kuhakikisha kwamba Rais Uhuru Kenyatta ameshinda uchaguzi huo.

“Wengi walifika katika afisi kuu za chama kulalamikia matokeo hayo, ila ilikuwa vigumu kuyatatua. Tulikuwa katika njiapanda, kwani baadhi ya maamuzi yalizidi uwezo tuliokuwa nayo. Yeye (Ruto) na watu wengine wenye ushawishi ndio walikuwa waamuzi wakuu,” akasema.

Baadhi ya wanasiasa walioshindwa kwenye teuzi hizo wamekuwa wakiulaumu usimamizi wa chama hicho, kama sababu kuu iliyochangia kushindwa kwao.

Miongoni mwao ni aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo, wanasiasa Kabando wa Kabando (Mukurwe-ini), Ndung’u Gethenji (Tetu), Zedekiah Buzeki (aliyewania ugavana Uasin-Gishu) kati ya wengine.

Bw Kabogo amekuwa akishikilia kwamba, ingawa alishindwa katika uteuzi huo, hakuamini matokeo yake.

“Ni kweli kwamba baadhi yetu tulishindwa kulingana na ufasiri wa chama, ila kulikuwa na ‘mkono’ wa watu wenye ushawishi kwenye uteuzi huo,” akasema.

Rais Kenyatta aliagiza chama hicho kufanya uteuzi mpya, baada ya duru ya kwanza kukumbwa na ghasia, kuchelewa kwa karatasi na madai ya mapendeleo kwa baadhi wawaniaji.