Habari MsetoSiasa

Murathe si wa hadhi yangu, asema Ruto

February 8th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto Ijumaa hatimaye aliguzia, japo kwa kudokeza, shutuma zilizoelekezwa kwake na aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa chama cha Jubilee Bw David Murathe.

Wakati wa kipindi cha maswali na majibu wakati wa mhadhara wa Chatham House, jijini London, Uingereza, Ruto alijaribu kuongea kuhusu shauku zilizoibuliwa kuhusu ufaafu wake kama mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2022.

Ripota mmoja wa gazeti la Financial Times alimtaka Dkt Ruto kujibu shutuma zilizoelekezwa kwake na Bw Murathe lakini akajibu hivi:

“Sijamjibu Murathe nchini Kenya. Na sioni nikimjibu nikiwa hapa barani Uropa.”

Akaongeza: “Murathe sio wa hadhi yangu.”

Naibu Rais alisisitiza kuwa amejitolea kuteleleza wajibu wake wa kuhakikisha kuwa Ajenda Nne Kuu za maendeleo ambazo serikali imeratibu zinatekelezwa, “pasi na kuingizwa siasa”.

Kuhusu siasa za 2022, Dkt Ruto alisema kuwa sio wajibu wake kuamua yule atakuwa mgombea wa urais wa Jubilee.

“Chama cha Jubilee na wanachama wake chini ya uongozi wa Rais, wataamua yule atakuwa mwaniaji urais,” akasema.

Naibu Rais aliomba radhi kufuatia hatua ya kufutiliwa mbali kwa mkutano wake na Wakenya wanaoishi London.

Kulingana naye, “Ilinibidi kurejea Kenya kwa wakati ili kumruhusu Rais kuondoka kwenda Ethiopia Jumamosi kwa sababu kikatiba, sisi wawili hatuwezi kuwa nje ya nchi kwa wakati mmoja.”

Hata hivyo, Dkt Ruto aliwaahidi Wakenya wanaoishi Uingereza kwamba atakutana nao atakaporejea huko wakati mwingine.