Makala

Muriu, Njuguna na Wasary waongoza ukaidi dhidi ya ushuru wa mavuno Murang’a

March 2nd, 2024 3 min read

NA MWANGI MUIRURI

KUPENDA ushuru kwa serikali ya William Ruto kwa sasa kumeelekezwa katika sekta ya kilimo ambapo analenga kuwa akipata asilimia  tano ya pato la wakulima.

Lakini juhudi hizo zilikumbana na pingamizi kali kutoka kwa wakulima wa parachichi ambao walikuwa wamekusanywa katika uwanja wa Kandara ili wachumbiwe, wakubali.

“Hatumtaki Zakayo juu ya mparachichi…tumekataa na aende aambiwe kwamba sisi hatutakubali parachichi itozwe huo ushuru,” mkulima mmoja akateta katika hafla hiyo ya Jumanne.

Maafisa wa Mamlaka ya Kukusanya Ushuru (KRA) walikuwa wamefika katika eneo hilo ambalo linasifika kuongoza uzalishaji maparachichi nchini.

Walikwua wamejihami kwa lugha tamu ya kuwachumbia wakulima wakubali kukatwa ushuru huo.

Mwenyekiti wa KRA Bw Antony Mwaura ni mzawa wa eneo bunge hilo la Kandara na ni kama alikuwa na fununu ya pingamizi hizo.

Hakufika kushuhudia wadogo wake wakiaibishwa kwa kukemewa na kuambiwa kwa mafumbo kwamba Zakayo mtoza ushuru hatakubaliwa kupanda juu ya mparachichi wowote wa eneo bunge la Kandara.

Kilichojiri ni maafisa wa KRA kukemewa, kunyimwa nafasi ya kuongea na hatimaye wakaagizwa watoke tu kwa usalama wao kutoka ukumbi huo wa hema.

“Inaonekana kwamba sisi sote tumekataa mwito huo wa kukatwa ushuru wa maparachichi. Mimi nikiwa kinara wa walio wengi katika bunge la Murang’a nitapeleka ujumbe kwa serikali ya Kaunti kwamba wakulima wetu wamekataa ushuru huo,” akasema Bw Kibe Wasary.

Wasary aliongeza kwamba kwa sasa mkulima amesononeshwa na gharama ya juu ya maisha na kile kidogo kinampa afueni mashinani hakifai kuvamiwa na ushuru.

Mkulima akikagua maparachichi yake katika Kaunti ya Nyeri. Wakuzaji zao hili Murang’a wamepinga kutozwa ushuru wa asilimia tano ya pato hili. Picha|Maktaba

Mbunge wa Kandara Bw Chege Njuguna pia alikuwepo na akatangaza kwamba hatakubali wakulima wake kuwekwa kwa mtandao wa ushuru wa mavuno.

“Sisi ni waajiriwa wa hawa watu ambao ndio wapiga kura. Wakisema wamekataa itabidi hata sisi tukubaliane nao. Kwa kauli moja tumekataa huo ushuru,” akasema.

Alisema kwamba “sio jana, sio leo na hata kesho…msimamo wetu ni uleule kwa wakati wowote ule kwamba hatutawahi kulipa kwa hiari ushuru wa maparachichi”.

Mbunge wa Gatanga Bw Edward Muriu aliapa kumfikishia ujumbe Bw Mwaura kwamba wakulima hata walio katika ujirani wake kijijini wamekataa kutozwa ushuru huo.

Alipendekeza ushuru huo utozwe wanaonunua maparachichi wala sio wakulima huku akifichua kwamba hata amemfahamisha Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kuhusu shida hiyo ya wakulima.

“Mimi niko na namba ya simu ya Bw Mwaura ambaye ndiye mwenyekiti wa KRA. Nitampigia na nimwelezee kwamba wakulima wake wamekataa ushuru huo,” akasema.

Kupenywa kwa madalali

Hali hatari katika mkutano huo ilikuwa kuonekana kupenywa na madalali wa sekta ya kilimo ambao walichukua fursa hiyo ya ukaidi kusema kwamba hata sheria mpya za mamlaka ya chakula na kilimo (AFA) kwamba uchukuzi wa maparachichi uwekewe vikwazo.

Mamlaka hiyo imesema kwamba maparachichi yakome kubebwa kiholela kupitia uchukuzi wa magari wazi, pikipiki, Tuk Tuk na baiskeli pamoja na mikokoteni.

Katika sheria ambazo zilikuwa zianze kutekelezwa Machi 2023, AFA ilisema kwamba ubebaji kiholea wa maparachichi ulikuwa ukiweka mavuno vidonda vilivyokuwa vikisababishia masoko ya ulaya kususia bidhaa kutoka Kenya.

Aidha, ilihofiwa kwamba uchukuzi kiholela ulikuwa unazidisha njama za wizi wa mazao mashinani ambayo husafirishwa usiku.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu alisema kwamba suala la ushuru linafaa kutenganishwa na lile la sheria za AFA.

“Hapo kwa ushuru naungana na wakulima kikamilifu na kabla wao wakubaliane na KRA, hizo harakati za kuwatoza ushuru shambani zinafaa zikomeshwe. Lakini kwa sheria za kupigana na kusambaratika kwa soko pamoja na wezi wa mazao shambani, madalali wakome kutuchezea akili,” akasema.

Bw Nyutu alisema kwamba “sheria za AFA zinalenga kuimarisha soko na mapato kwa manufaa ya wakulima kwa hivyo madalali ambao wamekuwa shida kuu kwetu waondoke na sheria mpya ianze kutekelezwa”.

Bw Muriu alisema kwamba “Gachagua amenihakikishia kwamba ataingilia kati kuhusu sheria hizo za AFA pamoja na ushuru huo ambao unadidimiza viwango vya faida kwa wafanyabiashara wa Mlima Kenya”.

[email protected]