HabariSiasa

Murkomen akome kuwahadaa Jumwa na Dori – ODM

February 6th, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

CHAMA cha ODM, Jumatano kimekataa rufaa ya mbunge wa Malindi Aisha Jumwa na mwenzake wa Msambweni Suleiman Dori ambao huenda wakafukuzwa chamani.

Hatima ya wabunge hao, iko mikononi mwa wajumbe wa chama baada ya Baraza Simamizi la Kitaifa (NGC) kuidhinisha watimuliwe chamani.

Kupitia wakili Kipchumba Murkomen ambaye ni seneta wa Elgeyo Marakwet, walimwandikia barua mwenyekiti wa ODM, John Mbadi, wakitaka wapatiwe fursa ya kujitetea mbele ya Baraza la Kitaifa la chama (NEC).

Walilalama kwamba uamuzi wa kuwatimua chamani ulifikiwa bila kufuata katiba ya chama na hawakupatiwa fursa ya kujitetea mbele ya kamati ya nidhamu na Baraza Kuu la Kitaifa la chama.

Hata hivyo, akijibu barua yao, Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, alisema kulingana na katiba ya chama hicho, uamuzi wa Baraza Kuu la Kitaifa la chama hauwezi kupingwa.

“Hakuna utaratibu wa kupinga uamuzi wa NEC mbele ya Baraza Simamizi la Kitaifa la chama (NGC),” inasema barua ya Bw Sifuna kwa Bw Murkomen.

Kulingana na Bw Sifuna, wabunge hao walionyesha kwamba hawaelewi katiba ya chama kwa kuandika barua hiyo.

“Wateja wako walijiaibisha kwa kudai kwamba wanafuata kikamilifu katiba ya chama ilhali hawana ufahamu wowote kuhusu katiba ya chama na ni ishara ya jinsi walivyojitenga nacho,” alieleza Bw Sifuna.

Taswira kamili ki kwamba Bw Murkomen anawahadaa Bi Jumwa na Bw Dori kwamba wana nafasi ya kukubaliwa tena katika chama cha ODM.

Alimtaka Bw Murkomen na wateja wake kusoma na kujifahamisha kikamilifu na katiba na kanuni za chama cha ODM ili kujiepusha na aibu ya kutafsiri visivyo katiba yake.

Kwenye barua yake kwa Bw Mbadi, Bw Murkomen alisema kulingana na katiba ya ODM, Bi Jumwa na Bw Dori hawakupatiwa nafasi ya kujitetea mbele ya kamati ya nidhamu na hata mbele ya Baraza Kuu la Kitaifa la chama hicho.

Walisema hakukuwa na kamati kamili ya nidhamu inavyosema katiba ya chama na kwamba walifika mbele ya mtu mmoja, Bw Fred Othouk.

“Hakukuwa na kamati kamili ya nidhamu iliyoundwa na kuidhinishwa na NEC kwa mujibu wa sheria. Mtu mmoja hawezi kuwa kamati,” walisema wabunge hao.

Wanasema uamuzi wa mtu mmoja ni kinyume cha sheria na hauwezi kutumiwa kama msingi wa kuwatimua chamani.

“Kwa hivyo, hakukuwa na uamuzi wa kuwasilishwa kwa NEC kwa sababu hakukuwa na kamati ya nidhamu ya kuupitisha,” wanasema.

Aidha, wanalaumu NEC wakisema haikuwa na wanachama wa kutosha kupokea na kuidhinisha uamuzi wa kamati ya nidhamu.

“Walalamishi hawakufika mbele ya NEC. Ukweli wa mambo ni kuwa hakukuwa na mkutano wa NEC kulingana na sheria,” wanasema.

Kulingana na wabunge hao, barua waliyoandikiwa na Bw Mbadi kuwataka waeleze kwa nini chama hangewachukulia hatua kwa uasi, haikufafanua malalamishi dhidi yao.

Wanasema walishirikiana na Naibu Rais William Ruto kwa moyo wa muafaka na wakakanusha kwamba walikuwa wakimpigia kampeni.

Kwenye barua yake, Bw Sifuna alisema uamuzi wa chama unadumu. “ Kwa sasa, suala hili ni la chama na wanachama wake, na hatutaruhusu wageni katika masuala ya ndani ya chama,” alisema.

Bw Murkomen alikuwa ameomba wabunge hao waruhusiwe kujitetea mbele ya NGC wakiandamana na wakili wao ndani ya muda wa miezi sita.