Makala

Murkomen alalama Dkt Ruto kapokonywa majukumu 'yote'

March 10th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen amedai kuwa Naibu Rais amapokonywa karibu majukumu yake yote ya Serikalini, kama sehemu ya mpango wa kuzima ndoto yake ya kuingia Ikulu mwaka 2022.

Seneta huyo wa Elgeyo-Marakwet anadai kuwa Dkt Ruto sasa ameagizwa “kuketi nyumbani” bila majukumu yoyote isipokuwa “kuhudhuria mikutano ya hafla za makanisa wikendi”.

“Naibu Rais anachukuliwa vibaya zaidi. Hata aliyeshikilia wadhifa wa Makamu wa Rais zamani alikuwa akipewa majukumu mahususi alivyofanyiwa Dkt Ruto katika muhula kwa kwanza wa utawala wa Jubilee ambapo aliongoza mikutano iliyohusiana na umeme, barabara, masuala ya vijana na elimu. Na kila mara aliwasilisha ripoti kwa Rais,” Bw Murkomen aliwaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Jumatatu alasiri.

Akauliza: “Mbona Naibu Rais hajapewa jukumu lolote ilhali yeye ni Naibu Rais aliyechaguliwa?”

Hata hivyo, Bw Murkomen aliwahakikishia wanahabari kwamba licha ya njama inayoendelezwa na baadhi ya watu wenye ushawishi serikalini, almaarufu ‘System’, Dkt Ruto yuko tayari kukabiliana na mahasidi wake.

Bw Murkomen alisema hayo siku mbili baada ya Naibu Rais mwenyewe kuzungumzia madhila yake alipohudhuria mazishi ya aliyekuwa Mkuu wa Ulinzi katika Afisi yake, Kipyegon Kenei katika eneobunge la Rongai, Kaunti ya Nakuru.

“Badala ya kuua afisa huyo ambaye hana hatia, walifaa kunilenga mimi. Nawaambia kwamba wakabilaane nami binafsi badala ya kuwaandama wandani wangu kila mara kwa kuwawekea kesi zisizo na msingi wowote,” Dkt Ruto akasema.

Marehemu Kenei alipatikana amefariki nyumbani kwake katika mtaa wa Imara Daima ikiwa ni siku moja kabla ya siku ambayo alikuwa anatarajiwa kutoa ushahidi kwa maafisa wa Upelelezi wa Jinai (DCI) kuhusiana na sakata ya ununuzi silaha feki.

Mhusika mkuu katika kashfa hiyo alitajwa kuwa ni Waziri wa zamani wa Michezo Rashid Echesa.

“Kwamba maafisa wa hadhi ya chini wanamkabili Naibu Rais kiasi hiki kunaibua maswali mengi bila majibu kuhusu wajibu wa Rais,” akasema.

Aliendelea kuuliza.

“Swali ambalo tunauliza ni je, Rais yuko wapi wakati huu ambapo naibu wake ananyanyaswa? Tunamtaka Rais Kenyatta azungumzie suala hili. Dkt Ruto anafaa kuhakikishiwa usalama wake,” akakariri Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet.

Lakini licha ya Bw Murkomen kudai kwamba Dkt Ruto amepokonywa majukumu yake, majuma mawili yaliyopita Ruto aliongoza mkutano wa Baraza Shirikishi kuhusu Bajeti (IBEC) katika makazi yake rasmi mtaani Karen.

Mkutano huo ulihudhuria na Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) Wycliffe Oparanya, Naibu wake Mwangi Wa Iria (Murang’a) na James Ongwae (Kisii).

Wengine waliohudhuria ni Msimamizi wa Bajeti (CoB) Margaret Nyakongo, mwenyekiti wa Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) Dkt Jane Kiringai na Waziri wa Fedha Ukur Yatani.

Ni katika mkutano huo ambapo ilikubaliwa kwamba serikali za kaunti zitengewe Sh316.5 bilioni katika mwaka wa kifedha ujao wa 2020/2021.

Huenda Bw Murkomen, na wandani wengine wa Dkt Ruto, wanakerwa na wajibu ambao Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’I wa kuwa mwenyekiti wa Kamati Shirika ya Mawaziri inayosimamia Utekelezaji wa miradi ya serikali kuu katika ngazi ya kitaifa na kaunti.

Kutia msumari kwenye kidonda, juzi Rais Kenyatta alimtuma Dkt Matiangi nchini Somalia kufanya mazungumzo na Rais Mohammed Abdullahi Farmaajo kuhusu kuhusu kisa ambapo wanajeshi wa nchini walivuka mpaka na kuingia Mandera.