Habari

Murkomen asema habanduki Jubilee

May 13th, 2020 2 min read

Na CHARLES WASONGA

SENETA wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen ameshikilia hatobanduka chama cha Jubilee na kusema ataendelea kuunga mkono Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto.

Akiongea saa chache baada ya kupokonywa rasmi wadhifa wa kiongozi wa wengi na kumlaumu vikali Rais Kenyatta kwa hilo, Bw Murkomen alisema halaumu yeyote kwa masaibu yake.

“Silaumu yeyote kwa kuondolewa kama kiongozi wa wengi katika seneti na sitaondoka Jubilee kwa sababu hiyo. Nitapambana mle ndani huku nikiendelea kutelekeza wajibu wangu wa kuikosoa serikali na kutetea ugatuzi,” Bw Murkomen amesema alipohojiwa na runinga ya Citizen Jumanne usiku.

“Na kwa kuikosoa serikali haimaanishi siwaungi mkono Rais na naibu wake bali ninachofanya ni kuwasaidia wawajibikie raia. Nimemuunga mkono Rais Kenyatta katika chaguzi za urais mara nne, tangu 2002. Na bado nitaendelea kuunga mkono serikali yake,” akaongeza.

Lakini awali katika seneti, Bw Murkomen alichemka kwa hasira huku akimrushia Rais cheche za lawama kwa kushinikiza mapinduzi dhidi yake.

“Ikiwa mafanikio makubwa ya Rais wa Kenya ni kuwaonyesha wananchi kwamba ‘nimemwondoa kiongozi wa wengi na kweli mimi ni mkubwa’ hiyo haina maana. Bw Spika tayari Rais ni mtu mkubwa lakini mimi ni mtoto wa skwota kutoka Embubut.

“Sasa mnamo wakati ambapo Murkomen si kizingiti, ewe Rais, wafanyie kazi wananchi wa Kenya. Na ukome kuwahadaa Wakenya kuhusu ahadi ulizotoa. Sasa sitakuwa kizingiti, rejesha katika bunge hili miswada yote uliyotia saini kinyume cha Katiba,” Murkomen akafoka.

Kuhusu migawanyiko iliyoko ndani ya Jubilee, seneta huyo amesema hali hiyo inachochewa na wanasiasa wachache pekee.

“Shida katika Jubilee inasababishwa na wafulani wachache, sio familia nzima ya wanachama ambao bado wako pamoja kama zamani. Wanasiasa hao wenye nia mbaya ndio wanawagawanya wanachama na viongozi,” Murkomen akasema.

Amesema amezungumza na Dkt Ruto kuhusu yaliyompata lakini “akaniambia nivumilie tu”.

“Naibu Rais aliniamba yaliyompata yeye na Rais Kenyatta wakati ule ambapo walipelekwa katika mahakama ya ICC ndiyo yaliyokuwa mabaya zaidi. Alisema haya ya seneti ni mambo madogo ambayo hayafai kunikosesha usingizi,” Murkomen akaeleza.

Hata hivyo, alisema kulingana na sheria za seneti angali “kiongozi wa wengi” kwa sababu taratibu za kisheria hazikufuatwa wakati wa kung’atuliwa kwake.

Katika mabadiliko yaliyofanywa wakati wa mkutano wa maseneta wa Jubilee na Kanu katika Ikulu Jumatatu, Seneta wa Pokot Magharibi Samuel Poghisio alipewa wadhifa wa kiongozi wa wengi. Nafasi ya kiranja wa wengi – mnadhimu – ilimwendea Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata baada ya Susan Kihika (Nakuru) kutemwa.