Michezo

Murkomen asema ni sawa Wakenya kukimbilia mataifa ya kigeni

Na GEOFFREY ANENE August 24th, 2024 2 min read

WAZIRI wa Michezo Kipchumba Murkomen ameunga mkono wanariadha kutoka Kenya kuendelea kutafuta riziki kwa kuwakilisha mataifa ya kigeni.

Asema haya alipokuwa akiwapa bendera wanariadha 22 watakaopeperusha bendera ya Kenya kwenye Riadha za Dunia za chipukizi chini ya umri wa miaka 20.

Bw Murkomen alitembelea timu hiyo kambini katika Kituo cha Michezo cha Kimataifa cha Kasarani jijini Nairobi Ijumaa.

“Dada yetu Winfred Yavi (bingwa wa dunia na Olimpiki) yuko nyuma yetu kikamilifu anapowakilisha taifa analokimbilia (Bahrain). Hata hivyo, anafaa kufahamu kuwa tutaendelea kuruhusu Wakenya kukimbilia mataifa mengine, lakini bado tutawabwaga tu,” akasema Murkomen.

Katika mkutano huo, Murkomen pia alitangaza kuwa washindi wa medali watakaowakilisha Kenya kwenye riadha hizo za dunia za U-20 mjini Lima nchini Peru juma lijalo watapokea donge nono.

Murkomen aliahidi kuwapa nyongeza ya Sh100,000 kwa kila mshindi wa medali ili kuwachochea zaidi kujituma kwenye mashindano hayo yatakayofanyika Agosti 27-31.

Kwa kawaida mshindi wa dhahabu, fedha na shaba katika Riadha za Dunia za chipukizi hutunukiwa Sh500,000, Sh350,000 na Sh150,000 mtawalia kupitia mradi wa serikali,

“Mimi kama waziri wenu nataka kuahidi kuwa yeyote atakayenyakua medali, mimi na rafiki zangu tutamuongeza Sh100,000,” akasema Murkomen.

Aliwaomba kuchukulia mashindano hayo kwa uzito kwa sababu Kenya itawategemea kwenye Michezo ya Olimpiki mwaka 2028 mjini Los Angeles, Amerika.

“Tunawategemea na tutatathmini matokeo yenu hata usiposhinda medali, lakini uwe umekimbia vyema. Tutatafuta ushauri kuona jinsi tutakusaidia kuendeleza taaluma yako. Baadhi ya wawakilishi wetu kwenye Olimpiki za Paris 2024 watakuwa wamestaafu ama kuingilia mbio nyingine wakati wa makala yajayo,” akasema Murkomen.

Aliahidi pia kusaidia Shirikisho la Riadha Kenya kuimarisha ujuzi wa baadhi ya makocha wetu na maafisa wengine ambao hawana ujuzi wa kisasa na teknolojia wa kukuza mabingwa wa dunia.

“Tutashughulikia hili kwa ushirikiano na shirikisho ili wapate kuimarika,” akasema.

Nahodha wa timu ya Kenya, Edmund Serem ameahidi kuongoza timu hiyo kuzoa medali mambo yakienda sawa.

“Makala haya hayatakuwa kama yaliyopita mjini Cali, Colombia wakati nafasi mbili za kwanza katika mbio za 3,000m kuruka viunzi na maji zilinyakuliwa na Ethiopia. Mathew Kosgey na mimi tumekuwa tukishirikiana vyema. Tulikuwa katika Riadha za Afrika na kushinda fedha na shaba,” akasema Serem.

Wanariadha hao 22 waliratibiwa kusafari mapema Jumamosi wakitumia ndege ya KLM.

Katika makala ya 2022 nchini Colombia, Kenya ilimaliza nambari nne nyuma ya Amerika, Jamaica na Ethiopia katika usanjari huo.

Walipata dhahabu tatu, fedha tatu na shaba nne.

Timu ya Kenya

Wanaume – Stephen Ndangiri (kutembea haraka 10,000m), Andrew Alamisi (5,000m), Koech Kibiwott (1,500m), Josphat Kipkurui (1,500m), Denis Kipkoech (3,000m), Ishmael Kipkurui (5,000m),  Kelvin Koech (800m), Phanuel Koech (800m), Matthew Kosgei (3,000m), Clinton Ngetich (3,000m), Edmund Serem (3,000m kuruka viunzi na maji)

Wanawake – Diana Chepkemoi (3,000m kuruka viunzi na maji), Mercy Chepkemoi (3,000m), Sharon Chepkemoi (3,000m), Sheila Jebet (5,000m), Janet Jepkemoi (800m), Marion Jepngetich (3,000m), Miriam Kibet (1,500m), Mary Nyaboke (1,500m), Sarah Moraa (800m).