Habari Mseto

Murkomen ashambulia Matiang'i, Kibicho bungeni

May 25th, 2019 1 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Wengi katika Bunge la Seneti, Kipchumba Murkomen, amedai kuwa Waziri wa Usalama wa Ndani na Katibu wake Karanja Kibicho wanaendeleza njama ya kuzima mipango ya Naibu Rais William Ruto kuwania urais mwaka 2022.

Na bila kuhimili madai yake kwa ushahidi, seneta huyo wa Elgeyo Marakwet alisema hatua ya hivi majuzi ya kuwapokonya bunduki Polisi wa Akiba wanaohuduma katika maeneo ya North Rift ni sehemu ya mipango ya kulemaza ndoto ya Dkt Ruto kuingia Ikulu.

Murkomen pia alielekeza kidole cha lawama kwa Inspekta Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai akimsuta kwa kile alichotaja kama kubadilisha sera zinazosimamia shughuli za Polisi wa Kitaifa wa Akiba (NPR) kwa lengo la kuadhibu ngome ya Naibu Rais.

“Huwezi kuhujumu usalama wa watu wa Bonde la Kerio kama njia ya kuhujumu ndoto ya urais ya Dkt Ruto,” akasema Alhamisi jioni alipokuwa akichangia mjadala kuhusu usalama katika kikao cha seneti.

Bw Murkomen pia alikasirishwa na madai yaliyohusishwa na Mbunge wa Tiaty William Kamket aliyesifu hatua ya kuondolewa kwa NPRs katika maeneo hayo.

“Napongeza Wizara ya Masuala ya Ndani kwa kuwapokonya silaha polisi hawa wa akiba kwani wangetumiwa kama wapiganaji wa Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2022,” Bw Kamket akasema kwenye ujumbe aliochapisha katika ukurasa wa mtandao wa Twitter.

Huku akionekana kukasirishwa na madai hayo ya Bw Kamket, Bw Murkomen aliitaka Wizara ya Masuala ya Ndani kutoa ufafanuzi la sivyo hatua yake ifasiriwe kama sehemu ya juhudi za kumhujumu Naibu Rais.

Kando na Bonde la Kerio, serikali pia imewapokonya silaha polisi wa akiba katika kaunti za Laikipia, Baringo, Pokot Magharibi, Turkana na Samburu.