Makala

Murkomen ashikilia hakuna jipya takwimu za ajali

April 21st, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

HUKU nduru zikitanda barabarani kupitia ajali kiholela zinazosababisha Wakenya wengi na hata wageni kupoteza maisha, Waziri wa Uchukuzi na Barabara Kipchumba Murkomen amejitetea kwamba hakuna cha kushangaza katika takwimu kwa kuwa hali imekuwa hivyo tangu mwaka 1963.

Waziri Murkomen alisema hiyo ni “hali ambayo imekuwepo kwa serikali zilizotutangulia sisi Kenya Kwanza”.

“Ni suala pasuakichwa kutoka kwa waziri mmoja hadi kwa mwingine. Hili halijachipuka katika utawala huu… ni hali ambayo imekuwa ikitusakama,” akasema Bw Murkomen.

Huku idadi ya waliokufa katika ajali tangu Januari 2024 ikizidi 1,200, Bw Murkomen alishikilia kwamba hali iko shwari kitakwimu na kile kinachofaa kuzua wasiwasi ni kama serikali iliyoko mamlakani itapuuza kuweka sera na mikakati maalum kuzima janga hilo la kilio barabarani.

“Hali ilivyo kwa sasa sio eti kuna ongezeko la ajali. Hali imekuwa hivyo kwa kuwa ni kero ambayo imekuwa nasi tangu tujinyakulie Uhuru,” akasema akiwa katika kaunti ya Murang’a.

Akiwa katika Shule ya Upili ya Mugoiri iliyoko eneobunge la Kiharu, alisema kwamba mikakati yote ambayo imekuwa ikiwekwa kuthibiti hali ya ajali barabarani haijakuwa ikizaa matunda.

“Kuna mfano wa Waziri (marehemu) John Michuki ambaye hurejelewa sana na wengi kwamba alichapa kazi katika sekta ya uchukuzi. Ndio, alifanya vyema kuleta ustaarabu wa wasafiri ambapo aliwahimiza wahudumu wa uchukuzi wawe wakipakia viwango fulani ndani ya matatu zao na pia kuwe na mikanda ya kiusalama. Lakini hakuweza kupunguza ajali za barabarani,”akasema.

Alisema kwamba kile kinachohitajika ni mbinu za kisasa ambazo zitatumia teknolojia za kufuatilia magari yanavyoendeshwa barabarani.

“Mimi niko na uhakika kwamba kile kitakachotuokoa sio kukemeana na kuelekezana kidole cha lawama mbali ni kuja pamoja na kushirikiana kuweka mikakati thabiti ya kuweka himizo kinachofanyika ndani ya magari barabarani,” akasema.

Alisema kwamba wizara yake iko katika harakati za kusaka mwanakandarasi ambaye ataweka masharti ya kiteknolojia ili wamiliki wa magari ya uchukuzi yakiwemo yale ya shule wawe wakiona kile kinachoendelea ndani ya gari likiwa linatumika.

“Tunataka hali kwamba ukiwa kwa mtambo wako uliounganishwa na gari kimawimbi, utamuona dereva na abiria wake. Utajua wakati gari linakiuka masharti ya spidi na hata dereva akianza kusinzia utamuona,” akasema Bw Murkomen.

Aliongeza kwamba shule ikiwa na ziara ya kusafirisha wanafunzi na shule hiyo iwe na mitambo hiyo ya kiteknolojia, “itakuwa rahisi kufuatilia kila sekunde ya safari hiyo”.

Vilevile, magari ya uchukuzi wa umma yakiwa na mitambo hiyo, akaongeza, itakuwa rahisi kwa mameneja wasimamizi kufuatilia mwendo kiasi kwamba “dereva akiongeza spidi au aegeshe kando mwa barabara ndio akavute bangi au kunywa pombe atakuwa akionekana na hatua ya kunusuru hali kuchukuliwa”.

Hata hivyo, kuna mambo kadha ambayo Bw Murkomen aliyatamka na ambayo yamewasinya Wakenya wengi hasa pale alijitenga na lawama akisema wizara ya Prof Kithure Kindiki ndio ya kulaumiwa katika ajali hizo ambazo zinatokea kila mara nchini.

Mnamo Jumatano, waziri huyo alisema hafai kulaumiwa, akiwataka Wakenya kuelekeza shutuma zao kwa idara ya Polisi wa Trafiki na Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA).

“Sio sawa kwa kulaumu Waziri wa Uchukuzi kila mara ajali inapotokea….. eti wanauliza, wapi waziri. Watu hata huingia ndani ya matatu iliyobeba abiria wengi kupita kiasi na kuchukua video na picha huku wakiuliza ‘yuko wapi Murkomen? Murkomen amefeli…,” akadai.

[email protected]