Habari za Kitaifa

Murkomen, Mwaura waonja hasira za vijana 70,000 katika X spaces


VIJANA kote nchini ambao wamekuwa wakiendeleza kampeni za kupinga Mswada wa Fedha wa 2024 sasa wanapanga upya mikakati yao huku wakishinikiza kuachiliwa kwa wenzao waliokamatwa katika maandamano ya Alhamisi.

Kupitia heshtegi #RejectFinanceBill2024, wanaendelea na mipango ya msururu mwingine wa maandamano Jumanne wiki ijayo.

Kuanzia Jumamosi, asubuhi, zaidi ya watumiaji 50, 000 wa mtandao wa X (zamani twitter) walishiriki jukwaa la mjadala kuhusu maandamano dhidi ya mswada huo tata huku wakipanga mikakati mipya watakayotumia katika maandamano ya wiki ijayo.

Maafisa wa serikali wakiwemo, Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen, Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura, Mwanamikakati ya Kidijitali Dennis Itumbi na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot, pia walishiriki katika jukwaa hilo la mjadala.

Mmoja baada ya mwingine, vijana hao walielezea masaibu yao kwa kukosa ajira baada ya kuhitimu kutoka vyuo mbalimbali vya mafunzo.

“Vijana wengi hawana la kufanya kujipatia riziki. Kwa upande mwingi kuna wanasiasa wachache kama Oscar Sudi wanaotembea na Sh20 milioni za kutoa katika harambee makanisani. Mbona utumie kiasi kama hicho cha pesa ambazo zinaweza kusaidia kuzalisha nafasi za ajira kwa maelfu ya Wakenya? Pesa hizo zinaweza kunitosha kulipa ujira kwa wafanyakazi kwa miaka 10,” akasema mtumiaji mmoja wa X Eric Amunga, almaarufu Amerix.

Wakati wa mazungumzo hayo, Waziri Murkomen alilumbana vikali na washiriki wakimtaka kuingilia kati kuwezesha kuachiliwa huru kwa mmoja wa watumiaji X anayejulikana kama Crazy Nairobian almaarufu Billy anayedaiwa kukamatwa.

“Masuala mnayoibua yana mashiko. Nimewasikia na nitawasilisha ujumbe huo kwa asasi husika,” Bw Murkomen akasema kisha akajiondoa kutoka mjadala huo.

Kampeni ya uhamasisho wa umma

Vijana hao pia wameafikia kuendelea kampeni kubwa ya uhamasisho wa umma nchini kwa lengo la kuongeza idadi ya vijana watakaojiandikisha kuwa wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Haya yanajiri huku vijana hao wakilalamika kupitia mitandao ya X na Tiktok kwamba marafiki zao wanatokomezwa na watu wasiojulikana.

Hali hiyo inaashiria urejeo wa enzi za zamani wa utawala wa rais wa pili nchini Hayati Daniel Moi ambapo wakosoaji wa serikali walitekwa na kutokomezwa au kutesa na nyakati zingine kuuawa.

Vijana hao wa kizazi cha sasa, maarufu kama Gen-Z, wamekuwa wakisambaza mitandaoni visa ambapo wenzao wamekuwa wakitokomezwa kwa njia isiyoeleweka.

Inadaiwa kuwa Billy (Crazy Nairobian) hajulikani aliko baada ya kukamatwa nyumbani kwake Ijumaa.

Naye mwanaharakati Boniface Mwangi aliweka ujumbe katika akaunti yake ya X kwamba watu wasiojulikana walijaribu kumteka nyara akiwa katika hifadhi ya maiti ya City, jijini Nairobi.

Baadaye aliwaarifu wafuasi wake mitandaoni kwamba angejiondoa kwa muda kuzuia kukamatwa kwake.

Katika kanda ya video iliyopakiwa mitandaoni na wakili James Wa Njeri, Bw Mwangi anaonekana ameketi nje ya Hifadhi ya Maiti ya City gari la kijani aina ya Subaru lilipofika hapo. Baadaye anaonekana akitoroka.

Aliyekuwa Jaji Mkuu wa Willy Mutunga alisema mwanaharakati huyo anasakwa na maafisa wa polisi.