MakalaSiasa

Murumbi mwanasiasa aliyejitolea kutetea wanyonge

March 18th, 2019 4 min read

NA KENYA YEARBOOK

JOSEPH Zuzarte Murumbi aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais wa pili nchini mnamo Mei, 1966 baada ya Rais Jomo Kenyatta kukosana na Makamu wa Rais, wakati huo, Jaramogi Oginga Odinga.

Awali, Murumbi alihudumu kama Waziri wa kwanza wa Mashauri ya Kigeni katika serikali ya kwanza iliyoundwa na Mzee Kenyatta baada ya Kenya kupata uhuru 1963.

Murumbi, alizaliwa mnamo 1911 katika eneo la Londiani, kaunti ya Kericho. Babake alikuwa mfanyabiashara wa asili ya kabila la Goa na mamake alikuwa Mmaasai.

Akihojiwa na wanahabari, Murumbi kama mtu aliyekuwa na uwezo wa kuzungumza lugha nyingi kama vile, Kimaasai, Kiingereza, Kihindustani, Kilumbwa na Kikuyu. Aliishi kwa miaka mingi nchini India.

Murumbi aliondoka nchini kwenda India mnamo 1917 alipokuwa na umri wa miaka sita pekee. Babake, Peter Zuzarte, alimsajili katika shule moja ya kimishenari katika jimbo la Bangalore. Alipomaliza masomo, aliajiriwa katika kiwanda kimoja cha kutengeneza barafu.

Baada ya miaka kadhaa, aliacha kazi nchini India na kurejea Afrika na kufanya kazi katika utawala wa Somalia kati ya mwaka wa 1941 na 1951. Na kati ya 1951 na 1957 alihudumu kama naibu katibu wa vuguvugu la Movement for Colonial Freedom.

Murumbi pia aliwahi kuhudumu kama Afisa wa Habari na Utalii katika Ubalozi wa Morocco jijini London, Uingereza.

Nchini Kenya alikutana na Pio Gama Pinto katika mkutano mmoja wa hadhara mnamo 1952, ambako Murumbi alijitokeza kuuliza maswali kutoka kwa mnenaji mmoja.

Urafiki kati yake Pinto ulikita na kushamiri kwa muda mrefu hadi Pinto alipouawa kwa kupigwa risasi mnamo 1965.

Pinto alimfahamisha Murumbi kwa wanachama wa kundi lililojulikana kama Kenya Study Group. Hili lilikuwa ni kundi dogo la wanasiasa, na watu wengine wa kawaida, ambao walikuwa wakikutana kujadilia changamoto za kisiasa za nyakati hizo.

Hivyo ndivyo, Pinto alivyomuingiza Murumbi katika siasa. Na serikali ya Ukoloni ilipotangaza Hali ya Hatari Nchini mnamo Oktoba 20, 1952 na kupelekea viongozi wa ngazi ya juu ya Chama cha Kenya African Union (KAU) kukamatwa, Murumbi alikuwa akihudumu kama kaimu katibu mkuu wa chama hicho.

Murumbi alisaka huduma za mawakili kwa viongozi hao wa KAU waliokamatwa wakati huo (viongozi sita ambao baadaye walifungwa Kapenguria), akiwemo Mzee Kenyatta.

Mnamo 1953, Murumbi aliondoka nchini na kwenda India ambako aliishi kwa muda wa miezi sita.

Katika kipindi hicho, Pinto alikuwa akimtumia vipande vya magazeti yenye habari na makala mbalimbali, kila wiki, kuhusu hali ya kisiasa nchini Kenya.

Murumbi alitumia habari hizo kuendeleza kampeni dhidi ya ukoloni nchini India na baadaye jijini Cairo, Misri na London, Uingereza. Kupitia usaidizi wa Pinto, aliweza kuifanya ulimwengu mzima kuwa na ufahamu kuhusu utawala dhalimu wa Uingereza kwa kuandika makala katika magazeti ya India kama vile The Chronicle.

Mnamo 1962, baada ya KAU kubadili jina na kuitwa Kenya African National Union (KANU), Murumbi aliteuliwa kuwa mwekahazina wake. Na katika uchaguzi uliofanyika mnamo 1963 alichaguliwa katika Bunge la Wawakilishi kuwakilisha eneo lililojulikana nyakati hizo kama Nairobi South.

Baraza la Mawaziri lilipobuniwa mwishoni mwa mwaka huo (1963), Murumbi aliteuliwa kuwa Waziri wa Serikali katika Afisi ya Waziri Mkuu, nyakati hizo akiwa Hayati Mzee Kenyatta.

Katika risala zake za rambirambi kuomboleza kifo cha Pinto, Murumbi alisema: “Alikuwa mwepesi kupinga vitendo vya ukiukaji wa haki. Ikiwa hizo ndizo zilikuwa sifa za mzalendo huyu ambaye alichukuliwa kama mkomunisti, basi nitawaambia waliomshutumu kwamba dhana yao kuhusu siasa zake, kwa hakika, ni potovu,”

Murumbi alikuwa kiongozi aliyekuwa na hamu ya kuhudumia taifa lake kwa heshima na taadhima. Lakini aligundua kuwa uadilifu na wema ni sifa ambazo hazileti ufanisi katika maisha ya mwanasiasa. Wale waliohudumu Serikalini walikuwa na mawazo tofauti kuhusu namna ya kuendesha shughuli za siasa na uongozi

Lakini Murumbi, ambaye alikuwa mwanasiasa aliyechukua ufisadi na siasa ya kuhujumiana, alikataa kufuata mienendo ya wanasiasa wa nyakati hizo na akajiuzulu mnamo Novemba, 1966. Hii ni baada ya kuhudumu kwa miezi saba pekee afisini, kama waziri.

Hata hivyo, Rais Kenyatta hakukumbatia hatua ya Murumbi kujiondoa serikalini.

Kwenye mahojiano na wanahabari kabla ya kufa mnamo 1990, Makamu huyo wa Rais wa zamani alielezea namna ambavyo Kenyatta “alipita mbele” yake bila kutamka neno alipomjulisha kwamba alitaka kujiuzulu.

Hata hivyo, hatimaye Murumbi alijiuzulu na nafasi yake ikachukulia na Daniel Arap Moi (Rais mstaafu). Na baada ya kifo cha Kenyatta mnamo 1978, Bw Moi alichukua hatamu za uongozi.

Kando na tofauti za kiitikadi kati yake na wanasiasa wa nyakati hizo, kujiuzulu kwa Murumbi, kwa kiwango kikubwa kulichangiwa na mauaji ya rafiki yake na mwelekezi, Pio Gama Pinto.

Mwaka mmoja baada ya Pinto kuuawa, Murumbi aliandika taarifa ya shukrani akimtaka kama rafiki wa maskini na watu wa tabaka la chini.

Akaandika: “Kote nchini, watu bado wanakumbuka ukarimu wake. Alitoa yote aliyokuwa nayo kwa watu maskini. Alipeana bila kuitisha chochote. Alikufa maskini.”

Murumbi alisema kuwa maadui wa Pinto walimshutumu kuwa mkomunisti. “Na hata kama alikuwa mkomunisti, kwa hakika katika Kenya inayozingatia misingi ya kidemokrasia, hiyo sio kosa ambalo hukumu yake ni kifo.” akasema.

Alimwelezea Pinto kama msoshiolisti ambaye aliishi na kutenda yale aliyoyaamini.

Murumbi alipenda kukusanya bidhaa za kisanaa. Hadi kifo chake, Murumbi alikuwa amekusanya jumla ya vitabu 50,000 na barua kadhaa rasmi.

Jumba la Kitaifa la Kuhifadhi Kumbukumbu (Kenya National Archives) limeanzisha maktaba yenye vitabu 8,000 vya kipekee (vilivyochapishwa kabla ya mwaka wa 1900) ambavyo vilipelekwa huko na Murumbi.

Murumbi aliasisi kituo cha sanaa kwa jina African Heritage kwa ushirikiano na mkewe Sheila na rafiki yake Alan Donovan. Kimegeuka kuwa kituo kikubwa zaidi cha sanaa barani Afrika.

Joe, alivyofahamika miongoni mwa marafiki zake, Murumbi aliwaazima watu wengi kutoka ng’ambo ambao walitaka kununua bidhaa kadhaa za kisanaa alizoweza kukusanya. Badala yake aliziuza kwa Serikali ya Kenya kwa bei nafuu.

Na alitoa masharti kwamba bidhaa hizo za kisanaa zihifadhiwe nyumbani kwake katika mtaa wa Muthaiga. Baadaye eneo hilo lingepanuliwa na kuwa Taasisi ya Mafunzo ya Masuala ya Afrika yenye maktaba, bweni na jiko.

Kwa bahati mbaya, Serikali iligawanya ardhi hiyo na kuwapa wastawishaji, kitendo ambacho kilishtua Murumbi. Inasemekana alishtuka zaidi pale alipotembelea eneo hilo na kupata kuwa wastawishaji walikuwa wamejenga majumba makubwa ya makazi.

Ilimlazimu kuhamia karibu na Mbuga ya Wanyama ya Maasai Mara, karibu na alikozaliwa mamake na kujenga makao. Rafiki yake, Alan Donavan aliitaja nyumba hiyo kama ya “kiajabu”.

Mnamo 1982, Murumbi alianguka ndani ya bafu na kuumia kwenye uti wa mgongo. Alisafirishwa hadi Nairobi kwa matibabu, lakini hatimaye hakufanikiwa kuweza kusimama wima na ikabidi atumie kiti cha magurudumu.

Murumbi alifariki (mnamo 1990) kutokana na mshtuko wa moyo. Naye mkewe, Sheila, alifariki mnamo mwaka wa 2000. Maiti zao zimezikwa katika makaburi ya City Park, zikikaribiana na kaburi la rafikiye, Pio Gama Pinto, kulingana na matamanio ya Murumbi.

Mnamo Machi 29, 2009, kituo cha kumbukumbu kwa jina Murumbi Peace Memorial, kilifunguliwa katika Bustani ya City Park, Nairobi.

Kimezingira makaburi ya Joseph na Sheila Murumbi na kijishamba kidogo chenye sanamu zilizotengenezwa na wasanii wa kale Afrika Mashariki. Kazi zao zimehifadhiwa katika kituo chenye bidhaa za kisanaa zilizokusanywa na Murumbi.

Kituo hicho cha kumbukumbu ni mojawapo ya maeneo machache ambako sanamu zilizotengenezwa na wasanii maarufu Afrika zinaweza kutizamwa mahala wazi.

Kwa hisani ya Kenya Yearbook Editorial Board; kenyayearbook.co.ke