Michezo

Murunga pazuri zaidi kuwa kocha wa Chipu baada ya wadhifa huo kuvutia wawaniaji 14

October 20th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

PAUL Murunga aliyewahi kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga saba kila upande, Shujaa, yupo pazuri zaidi kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, Chipu.

Murunga aliyeshindwa kumpiku Innocent ‘Namcos’ Simiyu kwenye kinyang’anyiro cha kuwa mkufunzi wa Shujaa mnamo Septemba, aliwahi kuwanoa vijana wa Chipu kwa miaka minne na kuwaongoza kufuzu kwa Olimpiki za Chipukizi zilizoandaliwa China mnamo 2015.

Isitoshe, mkufunzi huyo wa zamani wa Homeboyz ndiye aliyekuwa msaidizi wa kocha Benjamin Ayimba wakati Shujaa walipotwaa taji la Singapore Sevens kwenye kampeni za Raga ya Dunia mnamo 2016.

Murunga alikuwa pia sehemu ya maafisa wa benchi ya kiufundi walioongoza Shujaa kufuzu kwa Michezo ya Olimpiki iliyoandaliwa jijini Rio, Brazil mnamo 2016. Aliaminiwa kuwa kocha mkuu wa Shujaa mnamo 2018-19 baada ya Simiyu kujiuzulu.

Kwa mujibu wa Thomas Odundo ambaye ni Mkurugenzi wa Raga katika Shirikisho la Raga la Kenya (KRU), jumla ya wakufunzi 14 ndio waliokuwa wametuma maombi ya kuwania nafasi ya kudhibiti mikoba ya Chipu kufikia siku ya makataa (Oktoba 10).

Ingawa Odundo alikataa kuwafichua wawaniaji hao, alisema kwamba majina yao yamewasilishwa kwa Kamati ya Timu za Taifa (NSC) ambayo sasa itaandaa orodha fupi ya wagombezi na kuendesha mahojiano kabla ya kocha mpya kutangazwa rasmi mwezi ujao.

“Maafisa wengine wa kiufundi watakaoshirikiana na Simiyu kambini mwa Shujaa watafichuliwa rasmi mwezi ujao,” akasema Odundo.

Wadhifa wa kocha mkuu wa Chipu ulisalia wazi baada ya aliyekuwa mkufunzi mshikilizi kwa miaka mitano, Paul Odera kupokezwa mikoba ya timu ya taifa ya wanaraga 15 kila upande, Kenya Simbas mwishoni mwa Mei 2019.

KRU ilianza mchakato wa kutafuta kocha mpya wa Chipu mnamo Septemba 28 ilipotangaza kuwa inatafuta mkufunzi aliyehitimu kiwango cha pili cha ukufunzi wa kimataifa (World Rugby Level Two Certificate) katika kikosi cha wanaraga saba au 15 kila upande kwa mujibu wa viwango vya Raga ya Dunia (WR).

Kwa mujibu wa KRU, kocha huyo alitakiwa pia kuwa raia wa Kenya na ajivunie rekodi ya matokeo bora na tajriba ya angalau miaka minne ya kunoa kikosi cha raga katika kiwango cha klabu au shule.

Kibarua cha kwanza kinachomkabili kocha mpya wa Chipu ni kuongoza kikosi hicho kuhifadhi Kombe la Afrika kwa Chipukizi, Barthes Trophy. Kwa mwaka wa pili mfululizo, mshindi wa taji hilo atafuzu kwa raga ya dunia ya Junior Rugby World Trophy.

Kivumbi cha Barthes Trophy kilikuwa kiandaliwe jijini Nairobi kati ya Aprili 19-26, kabla ya kuahirishwa hadi mwakani kwa sababu ya janga la corona. Kenya imetiwa katika zizi moja na Zambia, Tunisia na Bukini.

Chini ya Odera, Chipu iliwaduwaza wapambe wa Afrika, Namibia kwa alama 21-18 katika fainali ya 2019 na kufuzu kwa raga ya dunia nchini Brazil.

Kwa mujibu wa mdokezi wetu katika KRU, Mitch Ocholla na Dominique Habimana ni kati ya wawaniaji watakaomtoa jasho Murunga. Ocholla ambaye kwa sasa anawatia makali vijana wa Impala Saracens, amewahi kudhibiti mikoba ya wasomi wa Chuo Kikuu cha Strathmore, Nakuru RFC na Shujaa (2010-12).

Hadi mwisho wa msimu wa 2019-20, Habimana ambaye ni mzawa wa Rwanda na raia wa Kenya, alikuwa kocha wa Kenya Harlequin. Amewahi pia kudhibiti chombo cha Nakuru RFC na kuwa msaidizi wa Kenya Simbas chini ya mkufunzi Jerome Paarwater kutoka Afrika Kusini.