Michezo

Musa Mohammed asaka klabu mpya akisubiri mkataba Nkana FC

June 18th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BEKI matata wa Harambee Stars, Musa Mohammed sasa anatafuta klabu mpya baada ya mkataba wake wa miaka miwili na Nkana FC ambao ni mabingwa mara 12 wa Ligi Kuu ya Zambia kutamatika.

Ingawa ni mwingi wa matumaini kwamba Nkana watarefusha muda wa kuhudumu kwake mjini Kitwe baada ya janga la corona kudhibitiwa, nahodha huyo wa zamani wa Gor Mahia anasema bado atakuwa radhi kunogesha Ligi Kuu ya humu nchini iwapo kuna kikosi kitakachomshawishi kujiunga nacho.

Mnamo Aprili mwaka huu, Musa alifichua kwamba huduma zake zilikuwa zikiwaniwa na vikosi vitano vya haiba kubwa barani Afrika. Hata hivyo, baadhi ya klabu hizo zilisitisha ghafla mchakato wa kumsajili baada ya corona kutikisa hazina zao za fedha.

Miongoni mwa klabu zinazohemea maarifa ya Musa ni Yanga SC ambao ni miamba wa soka ya Tanzania, Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini), Zamalek SC (Misri), St George (Ethiopia) na Kabwe Warriors (Zambia).

“Vinara wa vikosi hivi waliwahi kujadiliana na wakala wangu kuhusu uwezekano wa kunisajili miezi miwili iliyopita. Mkataba wangu na Nkana ulitamatika rasmi mnamo Mei 2020. Japo natarajia Nkana wanipe kandarasi nyingine msimu wa Ligi Kuu ya Zambia utakaporejelewa, bado itakuwa nafuu iwapo nitapata hifadhi mpya kwingineko,” akatanguliza beki huyo ambaye kwa sasa hujifanyia mazoezi katika uwanja Ligi Ndogo, Nairobi.

Musa amekiri kwamba kuchezea Gor Mahia ambao mabingwa mara 19 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), kulimwandaa vyema zaidi kwa soka anayoitandaza kwa sasa kambini mwa Nkana Red Devils. Nyota huyo alivalia jezi za Gor Mahia kwa kipindi cha miaka 10, tisa akiwa nahodha.

“Gor Mahia ni klabu kubwa inayojivunia mashabiki wengi ambao hukupa presha ya kuwa bora. Yeyote ambaye amewahi kuchezea Gor Mahia basi ana uwezo wa kutamba katika ligi yoyote barani Afrika,” akasema.

Musa alikuwa sehemu ya kikosi cha Harambee Stars kilichoshiriki fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019 nchini Misri.

Aliingia katika sajili rasmi ya Nkana mnamo Julai 2018 baada ya kuagana na FK Tirana ya Albania ambayo pia imewahi kujivunia huduma za Wakenya Francis Kahata, Eric ‘Marcelo’ Ouma na Kenneth Muguna ambaye kwa sasa anaviziwa na Simba SC ya Tanzania.

Chini ya unahodha wake, Harambee Stars waliambulia nafasi ya pili katika kipute cha kuwania ubingwa wa Hero International Cup nchini India mnamo 2018. Awali, alikuwa amewaongoza Stars kunyakua ubingwa wa Cecafa Senior Challenge Cup 2017 baada ya kuwazidi maarifa Zanzibar Heroes kwa mikwaju ya penalti uwanjani Kenyatta, Machakos.