Museveni afungua uchumi, japo kwa masharti makali

Museveni afungua uchumi, japo kwa masharti makali

Na XINHUA

KAMPALA, Uganda

RAIS wa Uganda Yoweri Museveni ametangaza kurejelewa kwa shughuli za kawaida nchini humo japo kwa masharti huku idadi ya maambukizi ya corona ikizidi kupanda.

Kwenye hotuba yake ya kukaribisha Mwaka Mpya, iliyopeperushwa moja kwa moja kupitia runinga za nchi hiyo, Rais Museveni alisema magari ya uchukuzi wa umma sasa yameruhusiwa kubeba idadi kamili ya abiria.

Hata hivyo, aliagiza kuwa abiria wote sharti wavae barakoa na kufuata masharti mengine ya kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa Covid-19.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa shule zote zitafunguliwa kuanzia Januari 10, 2022 na wanafunzi wenye umri wa miaka 18 na zaidi sharti wapewe chanjo.

Shule Uganda zimefungwa kwa karibu miaka miwili kufuatia mlipuko wa janga hilo Machi 2020.

Rais Museveni aliongeza kuwa maeneo ya burudani na michezo yarejelee shughuli za kawaida lakini sharti watu wazingatie masharti ya kuzuia msambao wa corona.

Maeneo hayo ya burudani pia yataruhusiwa kufanya kazi hadi saa za usiku.

Hata hivyo, kafyu itaendelea kuzingatiwa katika sekta ya bodaboda. Wahudumu wa pikipiki hizi za uchukuzi hawataruhusiwa kuhudumu nyakati za usiku.

Rais Museveni, hata hivyo alisema sekta nyingine za uchumi huenda zikafungwa tena ikiwa idadi ya maambukizi itaendelea kupanda.

Alieleza kuwa ikiwa asilimia 50 ya vitanda katika vitengo vya kuwahudumia wagonjwa mahututi (ICUs) na wadi za kuwahudumia wagonjwa wanaohitaji uchunguza wa karibu (HDU) vitatwaliwa na wagonjwa wa corona, sekta nyingine za uchumi zitafungwa tena.

“Japo tunafungua uchumi, aina mpya ya kirusi cha corona inaenea kwa kasi mno,” akasema.

Takwimu za wizara ya Afya zinaonyesha kuwa kiwango cha maambukizi ya aina hiyo ya kirusi cha Omicron kimepanda zaidi kwani jumla ya maambukizi 1,000 yamenakiliwa ndani ya siku kadhaa zilizopita.

Takwimu hizo zinaonyesha upimaji wa corona uliofanywa Desemba 30, 2021 ulibaini kuwa visa 1,658 vipya vilithibitishwa.

Idadi hiyo inafikisha 140, 737, idadi jumla ya visa vya maambukizi nchini humo tangu kisa cha kwanza kilipogunduliwa mnamo Machi 2020.

Rais Museveni walitoa wito kwa wananchi kuwajibika kibinafsi ili kufanikisha mpango wa kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo hatari.

Alisema baadhi ya maafisa wa serikali yake wameambukizwa corona kwa sababu ya kuzembea katika kufuatia masharti ya kujikinga.

You can share this post!

Everton wamsajili beki Mykolenko kutoka Ukraine

DINI: Tufuate nyayo za Mungu aliyetupa ‘Zawadi’

T L