Kimataifa

Museveni ahimiza wazazi kuwa washauri wa kwanza kwa wana wao

November 12th, 2019 1 min read

Na SAMMY WAWERU

MZAZI anapaswa kuwa mshauri wa kwanza kwa mtoto au watoto ili kuchangia ukuaji na maadili mema.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema ni jukumu la kila mzazi kuhakikisha mtoto amekua kwa njia ifaayo, katika malezi yake.

Akihutubu mapema Jumanne katika Kongamano la Idadi ya Watu na Maendeleo linaloendelea katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta, KICC, jijini Nairobi, Rais huyo amesema mienendo ya vijana itaimarishwa ikiwa wazazi watatumia pengo lao kama walezi kwa kuwashirikisha kwenye ushauri nasaha.

“Mimi ndiye mume, baba na babu wa wajukuu wangu pamoja na mpiganiaji uhuru shujaa (akimaanisha nchini Uganda), na ninahusishwa sana kwa ninachomiliki. Tunapaswa kushauri watoto wetu. Mimi ndiye mshauri wa karibu wa watoto na wajukuu wangu,” akafafanua Rais huyo wa Uganda.

Maelezo yake yameoonekana kulenga visa ambapo wazazi wananyooshewa lawama kwa kutelekeza majukumu yao katika malezi. Baadhi ya vijana, hususan kizazi cha kisasa wamepotoka kimaadili, wazazi wao wakitajwa kutoshughulika kuwalea ipasavya.

“Hakuna kisichohitaji ushauri au maelekezo katika jamii,” akasisitiza Rais Museveni.

Amesema serikali imejifunga nira kuimarisha wasichana na jinsia ya kike kwa jumla, ikiwa ni pamoja na kuangazia suala tete la mimba za mapema na vita vya kijinsia.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, alifungua rasmi kongamano hilo mapema Jumanne.

Aidha, juhudi za kuimarisha wanawake zinapigiwa upatu. Licha ya baadhi ya wadau husika kukosoa kongamano hilo, ukeketaji wa wasichana (FGM), mbinu za upangaji uzazi na mimba za mapema, ni miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa.

Mbali na Rais Kenyatta na Museveni, kiongozi mwingine aliyehutubu wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo ni Rais wa Ushelisheli Danny Faure.